Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeungana na taasisi nyingine za Serikali kushiriki Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane Kitaifa yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuwafikia wananchi na wadau mbalimbali kwa kutoa elimu na kupokea maoni.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa TARURA, Catherine Sungura amesema lengo kuu la ushiriki wa TARURA katika maonesho hayo ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu ya wakala huo, hasa katika usimamizi wa ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara mijini na vijijini.

“Tumejipanga kutoa elimu kwa wananchi juu ya maeneo mbalimbali tunayoyasimamia ikiwemo matengenezo ya kawaida ya barabara, uboreshaji wa maeneo korofi, shughuli za maabara, masuala ya mazingira na ushirikishwaji wa jamii,” amesena.
Amebainisha kuwa kupitia wataalamu waliopo kwenye banda la TARURA, wananchi wataelimishwa namna wanavyoweza kushiriki moja kwa moja katika shughuli za matengenezo ya barabara kupitia vikundi vya kijamii, hatua inayolenga kuongeza ushirikiano baina ya Serikali na wananchi katika kuboresha huduma za miundombinu.
“Tunawahamasisha wananchi na wadau mbalimbali kutembelea banda letu ili kupata elimu ya moja kwa moja kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana TARURA, hasa zile zinazolenga kuinua ushiriki wa jamii katika miradi ya barabara,” amesema.
Pia amewahimiza wananchi kutembelea banda la TARURA pamoja na mabanda mengine ya taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, yaliyo katika hema maalum la “Government Zone Pavilion 2”, ambapo elimu zaidi kuhusu taasisi hizo inatolewa.