Na Lucy Ngowi
MOROGORO: ZAIDI ya wakulima na maofisa ugani 2100 wamepatiwa elimu ya kanuni za kilimo shadidi cha mpunga kilichoboreshwa ili kuwawezesha kupata tija katika zao hilo.
Kilimo shadidi cha mpunga kinalenga kupunguza kiasi cha matumizi ya mbegu, maji pamoja na tija kuongezeka.
Mratibu wa Mradi huo wa kilimo shadidi cha mpunga, kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dkt. Atugonza Bilaro amesema idadi hiyo ya wakulima waliopata mafunzo hayo ni asilimia 108.8.

Dkt. Bilaro amesema mradi huo unatekelezwa katika, Halmashauri za Kilombero, Iringa, Chalinze, Bunda na Mbarali ambapo baada ya kufikia malengo kwa sasa umetanua wigo wa kuwafikia Wakulima katika Wilaya ya Kilosa,Morogoro.
Amesema TARI kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendelea na mkakati wa kuboresha uzalishaji wa zao hilo, kwa wakulima na moafisa ugani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ya Kilosa.

Bilaro amesema mafunzo hayo yamefanyika Disemba 17 hadi 21, 2024 kwa wakulima wa Skimu za Chanzuru, Rudewa, Ilonga, Kilangali na Mvumi ikiwa lengo ni kuwafikia wakulima 750 na maofisa ugani 10.
Naye Mkulima wa mpunga Skimu ya Chanzuru amesema miaka ya nyuma alipata mafunzo ya kilimo shadidi lakini ilikuwa vigumu kuendelea kutekeleza kwa muda mrefu kutokana na changamoto za kung’oa miche wakati wa kupandikiza.
Mkulima Petro amesema kupitia teknolojia ya Kitalu Mkeka aliyopata katika mafunzo hayo ni ya mafanikio sababu inajibu changamoto, hivyo kazi ya ung’oleaji itakuwa nyepesi.

Mradi huo unatekelezwa na TARI kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti ya Norway- Norwegian Institute of Bioeconomy research (NIBIO) na taasisi ya Utafiti ya Swamination (MSSRF) ya nchini India.