Na Lucy Ngowi
MOROGORO: TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia kituo chake cha Mlingano, imeonesha mafanikio makubwa katika utafiti na uvumbuzi wa kisasa unaolenga kuboresha sekta ya kilimo nchini.

Mratibu wa Utafiti na Ubunifu kutoka TARI Mlingano, Dkt. Sibaway Mwango amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa Habari hizi katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Morogoro.
Dkt.Mwango amesema kupitia maonesho ya kitaifa ya kilimo yanayoendelea, TARI Mlingano imejikita kuonesha mafanikio ya kipekee katika uzalishaji wa miche bora ya mkonge, utunzaji wa vinasaba vya viungo adimu pamoja na uboreshaji wa huduma za upimaji wa udongo kupitia maabara inayotegemewa na taifa.

Kwa upande wa mkonge, amesema TARI Mlingano imefanikiwa kuzalisha miche bora milioni 2.5 ya mkonge na kusambaza kwa wakulima katika maeneo mbalimbali ya nchi.

“Mbegu chotara ya mkonge aina ya H11648, ambayo kwa sasa ndiyo msingi wa uzalishaji wa mkonge nchini, imefanyiwa utafiti na wataalam wa taasisi hiyo,” amesema.
Amesema miche hiyo inapatikana katika banda la TARI Mlingano kwenye maonesho hayo na wakulima wamehamasishwa kufika kujionea mbegu hiyo iliyoimarishwa.
Kwa sasa, TARI Mlingano ina uwezo wa kuzalisha miche ya mkonge hadi milioni 3 kwa mwaka, ingawa mahitaji ya kitaifa yanazidi miche milioni 12. Ili kuziba pengo hilo, taasisi hiyo inaendelea na ujenzi wa maabara ya kisasa ya tissue culture ambayo inatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu wa fedha.
“Maabara hiyo itakapokamilika, itazalisha zaidi ya miche milioni 10 kwa mwaka, hatua itakayosaidia kutatua kabisa changamoto ya upatikanaji wa miche bora ya mkonge nchini,” amesema.
Mbali na mkonge, TARI Mlingano pia ina jukumu la kuhifadhi na kuendeleza vinasaba vya viungo muhimu vya kiuchumi ikiwemo karafuu, cocoa, mdalasini, tangawizi, iriki na all spices.

Amesemq katika eneo la zaidi ya hekta 30, taasisi hiyo imehifadhi vinasaba hivi vyenye thamani kubwa kwa uchumi wa viwanda na masoko ya kimataifa.
“Kupitia vinasaba hivyo, wameweza kuzalisha miche bora na kusambaza kwa wakulima. Mwaka huu pekee, TARI Mlingano inazalisha miche 350,000 ya karafuu na kuisambaza katika halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro,” amesema.
Pia amesema eneo la teknolojia na huduma za sayansi ya udongo, TARI Mlingano imejivunia kuwa na Maabara Kuu ya Udongo ya Tanzania, ambayo kwa sasa ipo kwenye hatua za mwisho za kufanyiwa ithibati ya kimataifa.

Amesema maabara hiyo imekuwa mhimili muhimu kwa wakulima, watafiti na sekta binafsi, lakini kwa muda mrefu wakulima wakubwa walilazimika kupeleka sampuli zao za udongo Afrika Kusini kutokana na ukosefu wa uhakika wa ubora wa huduma za kitaifa.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwango, maabara hiyo inatarajiwa kuongeza uwezo wake wa kupima afya ya udongo kutoka sampuli 3,000 kwa mwaka hadi zaidi ya 30,000.
“Hii itatoa fursa kubwa kwa wakulima kupata takwimu sahihi kuhusu afya ya udongo wao, na hivyo kufanya maamuzi ya kilimo kisayansi na chenye tija zaidi,” amesema.v
TARI Mlingano kwa sasa imejikita kuhakikisha matokeo ya utafiti yanamfikia mkulima moja kwa moja, ikiwa ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa miche bora, huduma za uchunguzi wa udongo na kuendeleza vinasaba vya mazao ya viungo. Hatua hizi zinaifanya taasisi hii kuwa kitovu cha mageuzi ya kilimo chenye tija nchini Tanzania.