Na Mwandishi Wetu
CAPE TOWN – AFRIKA KUSINI: TANZANIA inaendelea kutangaza fursa mbalimbali za uwezeshaji katika Sekta ya Nishati ili kuifungua nchi Kimataifa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amesema hayo leo Novemba tano katika Kongamano la Wiki ya Nishati 2024 linalowakutanisha
wadau wa nishati ya mafuta, gesi asilia na nishati jadidifu kutoka barani Afrika na nchi nyingine duaniani.
Amesema utangazaji huo wa nchi ya Tanzania, unaenda sambamba na mpango wa kunadi vitalu vilivyo wazi nchini kwa ajili ya utafutaji wa mafuta na Gesi Asilia.
“Tanzania inatumia kongamano hili kueleza fursa nyingine za uwekezaji katika vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia alivyopewa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na fursa zilizopo katika mkondo wa kati na wa chini wa petroli ikiwemo miradi ya Mini LNG.,” amesema.
Pia amesema Mamlaka ya Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) itakuwa na banda la maonesho kwa kushirikiana na TGS, huko masuala mbalimbali ya mkondo wa juu wa petroli yataoneshwa pamoja na maandalizi ya duru ya tano ya kunadi vitalu vya utafutaji mafuta na gesi asilia vilivyo wazi nchini.
Vile vile amesema kongamano hilo litavutia washiriki wengi duniani kwa kuwa limekidhi mwelekeo wa dunia wa kuondokana na nishati chafuzi za mazingira.
Amesema washiriki kutoka Tanzania wataweza kukutana na kampuni mbalimbali za mafuta na gesi asilia duniani ikiwemo Schlumber Company Ltd.
Kwa mwaka 2024, kongamano hilo ni la 30 linafanyika kuanzia Novemba nne hadi nane likihusisha wadau wa nishati zote duniani.