Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali itaendelea kujiimarisha kidiplomasia na itaongeza nguvu zaidi ili kuwawezesha watanzania wengi kupata fursa mbalimbali katika jumuia za kimataifa.
Amesema serikali imefanikisha kuimarisha ushirikiano baina ya nchi washirika, sasa mafanikio yanaonekana.
Majaliwa amesema Rais Samia ameonesha
nia njema katika kipindi chake cha miaka mitatu na nusu kwa kujenga diplomasia na mahusiano katika sekta mbalimbali na nchi nyingi duniani.
Amesema hayo leo Agosti nne, 2024
alipokutana na Mkurugenzi Mkuu Mteule wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika (WHO) Dkt. Faustine Ndungulie, Ofisini kwake Mlimwa Jijini Dodoma.
“Tunaamini kazi kubwa tulizozifanya katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya kumpata Spika wa Umoja wa Mabunge duniani haikuwa kazi ndogo, na tena tumepata Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika,” amesema.
Majaliwa amesema serikali itaendelea kumuunga mkono Mkurugenzi huyo katika utekelezaji wa majukumu yake mapya.
“Wakati wote Waziri wa Afya atakuwa karibu nawe kuhakikisha kwamba sera zetu zinaenda sambamba na malengo ya WHO, kwa uwepo wako sisi lazima tuwe mstari wa mbele kuhakikisha kwamba tunakuunga mkono kwa mipango yetu ya afya ndani ya nchi,”.
Kwa upande wake Mkurugenzi huyo Mtarajiwa wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika Dkt. Faustine Ndungulile amemshukiru Rais Samia kwa kumuunga mkono na kufanya ushawishi wa kidiplomasia ili kufanikisha ushindi huo.
“Kwa upekee sana ninamshukuru Rais Samia kwa jitihada zake kubwa katika kufanikisha ushindi huu kwa ushawishi wake kwenye jumuia za kimataifa pia nawashukuru viongozi wengine wa Serikali, Bunge na wadau wote,” amesema.