Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimetoa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kwa wanawake wa kijiji cha Misufini, wilayani Kibaha mkoani Pwani, ili kuwawezesha kiuchumi na kuchochea uhifadhi wa mazingira kupitia uzalishaji na usindikaji wa mazao ya nyuki.
Akizungumza wakati wa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari, Mkurugenzi wa TAMWA, Rose Reuben, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa kuanzisha mradi wa mfano wa ufugaji wa nyuki katika shamba la shirika hilo lililopo Misufini.
“Shamba letu liko Misufini na tunataka majirani zetu hasa wanawake wanufaike na mradi huu. Lengo ni kuwawezesha kiuchumi kupitia shughuli endelevu,” amesema
Amesema nyuki ni chanzo muhimu cha kipato kwa kutumia rasilimali zilizopo kwenye mazingira ya asili, huku akieleza kuwa asilimia 80 ya shughuli za kilimo nchini hufanywa na wanawake.
“Kupitia ufugaji wa nyuki, wanawake watapata fursa ya kujipatia kipato endelevu kutoka kwa mazao kama asali, masega, chavua na gundi,” alieleza.
Kwa hatua ya awali, TAMWA inatarajia kuweka mizinga 200 ya nyuki kwenye shamba hilo kama sehemu ya utekelezaji wa mradi.
Naye Ofisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Christina Samweli, amesema nyuki wana mchango mkubwa katika maisha ya binadamu, si kwa asali pekee bali pia kwa mazao mengine yenye thamani kubwa kiafya na kibiashara.
“Mazao ya nyuki kama chavua na gundi ni tiba na chakula. Lakini bado jamii nyingi hazijafahamu fursa hizi,” amesema.
Amesema wanawake kuchangamkia mafunzo hayo kwa kuwa yanatoa maarifa muhimu ya kutumia ardhi kwa tija bila kuharibu mazingira.
Aidha, ufugaji wa nyuki umetajwa kuwa ni shughuli rafiki kwa mazingira kwani hauhitaji ukataji wa miti wala matumizi ya kemikali, bali huchochea uhifadhi wa misitu na mimea.
Kupitia mradi huo wanawake wa Misufini wanatarajiwa kuwa mfano wa kuigwa katika matumizi bora ya rasilimali asilia kwa ajili ya maendeleo ya jamii na uhifadhi wa mazingira kwa vizazi vijavyo.
–