Na Lucy Lyatuu,Tanga
TAASISI ya TABIO, inayohimiza utunzaji wa bayoanuai, kwa kushirikiana na Kikosi Kazi cha Mbegu Asili Tanzania, imewaasa wakulima kutunza na kuendeleza mbegu pamoja na mazao ya asili ili kuimarisha ustahimilivu wa mifumo ya chakula dhidi ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo athari zinazoweza kujitokeza wakati wa El Niño.
Wito huo umetolewa katika wiki ya Chakula duniani inayofanyika jijini Tanga, ambapo wadau hao wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mbegu za asili na kulinda bayoanuai kwa ajili ya kuimarisha usalama wa chakula.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Msimamizi Wa Mradi Wa TABIO, Daud Manongi, amesema utunzaji wa mbegu za asili ni muhimu katika kuhakikisha wakulima wanaendelea kuwa na rasilimali za kilimo zinazoweza kuwasaidia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Ameeleza kuwa mbegu za asili ni sehemu muhimu ya urithi wa jamii na zina mchango katika kuhifadhi bayoanuai, kuendeleza maarifa ya jadi na kuimarisha mifumo ya uzalishaji wa chakula inayozingatia mazingira.
Aidha, amesema juhudi za kuhifadhi na kuendeleza mbegu za asili zinapaswa kupewa kipaumbele ili wakulima na jamii kwa ujumla wawe na uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto za tabia nchi na kulinda uzalishaji wa chakula.
Ushiriki wa TABIO na Kikosi Kazi cha Mbegu Asili katika maadhimisho hayo ni sehemu ya kuunga mkono kampeni kubwa ya “Mbegu ni Uhai,” inayohusishwa na Mtandao wa Uhuru wa Chakula Barani Afrika (AFSA).

Kampeni hiyo inalenga kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa mbegu za asili, kulinda bayoanuai na kuimarisha mifumo ya chakula inayozingatia haki na mahitaji ya jamii.
Kupitia kampeni hiyo, wakulima wanahimizwa kuhifadhi mbegu zao, kuendeleza kilimo cha mazao mbalimbali na kubadilishana maarifa kuhusu namna bora za kutunza rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Amesema wiki ya Chakula inaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa kilimo na chakula, kuelimisha umma na kuhamasisha hatua za pamoja za kulinda bayoanuai na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!