Na Danson Kaijage
TAASISI zote za Serikali zimetakiwa kuingia katika mfumo wa kielektroniki utakaowezesha mifumo ya Serikali kuwasiliana (GovESB), na ambazo hazijaingia katika mfumo huo zimepewa muda wa siku 30 ziwe zimejiunga.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa maagizo hayo kwenye kilele cha Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma, alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Park Jijini Dodoma.

Amesisitiza taasisi zote za umma ambazo hazijajiunga na mfumo huo mwisho ni Julai 30 mwaka huu.
Amesema mfumo huo una faida kubwa katika utumishi wa umma kwa kuwa utasaidia kurahisisha utendaji, kutoa taarifa kwa wakati, kuondoa makosa ya kibinadamu katika kuwahudumia wananchi pamoja na kuwabana wala rushwa.
“Nimefurahi kujulishwa kwamba jumla ya mifumo 223 kutoka kwenye taasisi 185 imeunganishwa na kusomana,” amesema.

Ametoa wito kwa taasisi zote za umma zenye mifumo na zinazoendelea kubuni mifumo zihakikishe mifumo hiyo inasomana na inaweza kubadilishana taarifa kupitia mfumo huo wa GovESB ikiwa ni njia mojawapo ya kuendelea kuboresha huduma za Serikali.
Pia ameitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kuhakikisha mifumo iliyounganishwa inaendelea kubadilishana taarifa.
“Lakini pia kila anayeingia jiridhishe kuwa anaweza kuwasiliana na wengine wote waliomo ndani, mmenieleza na mmesema kwamba ndivyo ilivyo, nasisitiza kwamba hakikisheni hiyo mifumo inasomana na inabadilishana taarifa,” amesema.

Pia ametoa wito kwa watumishi wa umma kuzingatia miiko na maadili ya utumishi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingitia Sera na Sheria kwa manufaa na maendeleo ya Taifa letu.
“Nitumie nafasi hii kuwapongeza sana watumishi wote wa umma nchini, niwahikishie kuwa serikali ya awamu ya sita iko pamoja nanyi. Fanyeni hivyo kwa ajili ya manufaa na maendeleo ya Taifa letu,” amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema Tanzania imetambulika kimataifa ambapo mwaka 2022 Benki ya Dunia ilifanya utafiti kuhusu ukomavu wa matumizi ya teknolojia duniani katika utoaji wa huduma za Serikali na ushirikishwaji wa wananchi.
Amefafanua kuwa ripoti ya utafiti huo iliyotolewa Machi, 2023 ilibanisha kuwa Tanzania imefanikiwa kupanda daraja kutoka kundi B hadi kundi A na kushika nafasi ya 26 duniani, nafasi ya puli Afrika na nafasi ya kwanza katika nchi za Afrika Mashariki.
Katika tukio hilo,Majaliwa alizindua mifumo miwili ambayo ni GovESB Pamoja na Mfumo wa e-Wekeza unaomwezesha Mtumishi wa Umma kuwekeza katika Mfuko wa Faida (Faida Fund).
Siku ya Utumishi wa Umma husherehekewa Juni 23 kila mwaka na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kwa lengo la kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla
Mwisho..