Na Lucy Ngowi
GEITA: MKUU wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, amezitaka taasisi za elimu mkoani Geita kuanzisha programu maalum ya utoaji wa maziwa shuleni ili kuongeza kasi ya unywaji wa maziwa miongoni mwa wanafunzi.
Komba amesema hayo alipozungumza katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Martine Shigela.

Komba amesema ni muhimu programu hiyo ikatekelezwa sambamba na mpango wa lishe shuleni kwa lengo la kuboresha afya za wanafunzi.
Amewataka Maofisa Elimu wa mkoa kujipanga kutekeleza mpango huo huku akiwaasa wazazi na walezi kuhakikisha maziwa yanapatikana katika familia ili kuendeleza utamaduni wa unywaji wa maziwa.
Naye Mwakilishi wa Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Deorinidei Mng’ong’o, amesema jumla ya lita 240 za maziwa zimesambazwa kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum mkoani Geita, huku wanafunzi 300 kutoka vituo vya kulelea yatima wakinufaika na mpango huo.

Mpaka sasa Bodi hiyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefika mikoa 11 nchini, ambapo shule 218 na wanafunzi wapatao 120,000 wamefikiwa na programu hiyo ya unywaji wa maziwa shuleni.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika mkoani Geita yamebeba kaulimbiu isemayo: ‘Kwa Matokeo Mazuri Shuleni na Afya Bora, Maziwa ndio Mpango Mzima.’

