Na Lucy Ngowi
TANGA: WAFUGAJI wa ng’ombe wa maziwa jijini Tanga, wameshukuru kwa kupata elimu ya jinsi ya umuhimu wa usafi wakati wa kukamua ng’ombe ili kuepusha kupata homa ya kiwele iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Mfugaji kutoka Kata ya Mzizima, Winnie Lema amesema kupitia elimu hiyo waliyopewa kuhusu homa ya kiwele na SUA, kupitia mradi unaofadhiliwa na Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo na Utafiti cha Canada (IDRC), imewangozea uelewa kwa kiwango kikubwa.
Amesema awali hawakuwa na elimu hiyo, hivyo imewawezesha kuyajua makosa waliyokuwa wakiyafanya bila kujua.
Mtafiti Kiongozi wa Mradi huo, Profesa Gaymary Bakari amesema mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na wafugaji 47, yana lengo la kutoa mrejesho kwa wafugaji na kutambua changamoto wanazokumbana nazo.
“Mafunzo haya ni sehemu ya tathmini ya hali halisi ya homa ya kiwele katika mkoa wa Tanga, baada ya kufanya utafiti wa awali, sasa tumeleta mrejesho na kuwasikiliza wafugaji ili kuelewa changamoto na namna ya kuimarisha tiba tunayoendelea kuibuni,” amesema.
Naye Ofisa Mifugo kutoka Halmashauri ya Jiji la Tanga, Dkt. Rashid Chonga Nasoro, ameipongeza SUA kwa kupeleka elimu hiyo kwa wafugaji.
“Mafunzo haya yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza athari za homa ya kiwele. Tumejifunza njia sahihi za kukinga na kudhibiti ugonjwa huu,” amesema.
Mradi wa NANO COM unatekelezwa katika mikoa mitano nchini ambayo ni Tanga, Iringa, Mbeya, Njombe na Arusha. Tafiti katika maeneo haya zinalenga kubaini vyanzo vya homa ya kiwele na kubuni tiba mbadala kwa ajili ya wafugaji nchini Tanzania.