Mkurugenzi Mtendaji atoa ahadi kwa wafanyakazi, wachimbaji wadogo
Na Lucy Ngowi
GEITA: MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Venancy Mwase, amewataka wafanyakazi wa shirika hilo kuendelea kuwa wabunifu, waaminifu na kujituma zaidi katika majukumu yao, huku akiahidi kuwashika mkono kwa karibu kutokana na juhudi na mafanikio wanayoendelea kuonyesha.
Amezungumza hayo Septemba 28, 2025, wakati wa kufunga Maonesho ya Nane ya Sekta ya Madini yaliyofanyika Geita.

Amewapongeza wafanyakazi wa STAMICO kwa kazi nzuri wanayoifanya akisema,”Kushukuru ni jambo jema, lakini niwaambie mnafanya kazi nzuri sana,”.
Ameahidi kuwasaidia wachimbaji wadogo hususani wanawake kwa kugawa pampu za maji kwa kusema,
“Nimeahidi mwenyewe. Kamilisheni utafiti wa mahitaji, tutaanza kutoa kwa awamu hadi akina mama wote waondokane na changamoto hiyo.”

Pia amesema agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kutenga mashine inayotumika kwa ajili ya utafiti au uchimbaji wa madini (rig), moja mahsusi kwa wanawake tayari limeanza kutekelezwa, vifaa vikiwa karibu kukamilika.

“Tunafuata utaratibu ule ule: Crasha iko, shed iko, na sasa tunatafuta vijana wa kusaidia vikundi hatua kwa hatua,” amesema.
Mwase amesena STAMICO inaendelea kujipanga kuhakikisha inaongeza msaada mkubwa kwa wafanyakazi na wadau wa sekta ya madini.
“Kila kidogo Serikali inachotoa kupitia STAMICO, mafanikio yake yanaonekana. Kwa nini msipewe kikubwa? Hatujawahi kuangushwa.” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA), Salma Ernest ametoa shukranikwa Mkurugenzi wa STAMICO kwa kusaidia utekelezaji wa Mradi wa Malika wa Madini mkoani Geita.
Mradi uliowezesha wanawake kufanyika kwa tafiti za kijiolojia, kuundwa kwa vikundi vipya vya wanawake wachimbaji, Kutoa elimu kwa zaidi ya wanawake 640, Kugawa jokarasha tano kati ya 20 zilizopo nchini, na kusaidia ushiriki wa wanawake kwenye maonyesho ya mwaka huu 2025.
“Tumetembelea mabanda yote, tumetambulika sisi ni nani na tunafanya nini. Tumekutana na mabenki na makampuni makubwa haya yote yametokea kwa sababu umetufungulia njia,” amesema.