Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WANA TAALUMA Vyuo Vikuu duniani wanaamini ili kupata majawabu ya matatizo yaliyopo kwenye jamii inawapasa kufanya tafakuri za kina pamoja na mijadala.
Mhadhiri Mwandamizi Kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM), Sosholojia na Anthropolojia, Dkt. Richard Sambaiga amesema hayo wakati wakitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu Kongamano Juu ya Uhuru wa Wana Taaluma katika Afrika.

Amesema,” Kama vyuo vikuu barani Afrika na ulimwenguni, kazi yetu kubwa ni kufanya tafiti, kufundisha wanafunzi na kutafuta majawabu ya matatizo.
” Tunaamini peke yetu bila sauti na kuungwa mkono na wadau wengine, hatutaweza ila tukiendelea kukumbushana tunaweza kutoka hapa tulipo na kwenda hatua nyingine,”.
Amesisitiza matatizo yanayoikabili jamii yanahitaji majawabu yatokanayo na tafiti mbalimbali wanazozifanya.
Naye Mhadhiri Mwandamizi UDSM kutoka Ndaki ya Sayansi ya Jamii, Dkt. Ng’wanza Kamata amesema kongamano hilo litaanza Aprili 29 hadi Mei 2, 2025 limeandaliwa na Ndaki ya Sayansi za Jamii UDSM kwa ushirikiano na Kanseli ya Maendeleo ya Utafiti katika Sayansi za Jamii (CODESRIA).
Amesema mkutano huo utafunguliwa na Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson na utahudhuriwa na wana taaluma, wanazuoni na washirika wengine zaidi ya 200 kati ya hao 100 watatoka vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za Afrika na nje ya Bara, 100 wengine watatoka Tanzania.
“Baada ya uzinduzi itafuatia mijadala ya kitaaluma ambayo itatanguliwa na uwasilishaji wa mada mbalimbali zipatazo 80 zitakazo wasilishwa katika vikao na majopo,” amesema.
Amesema mada hizo zitazungumzia uhuru wa wana taaluma katika muktadha wa nguvu kinzani, dola ba wana taaluma, vyuo vya elimu ya juu na uhuru wa wanataaluma, urasilimishaji wa vyu vikuu na nyinginezo.
Kwa upande wake, Meneja wa Program CODESRIA Dkt. Bertha Kibona amesema mpango wao mkubwa ni kusaidia taaluma kwenye sayansi za jamii Afrika.
Amesema kazi yao ni kuhakikisha uhuru wa taaluma unakuwepo ambapo kwao ni jambo la kipaumbele.