Na Lucy Ngowi
DODOMA: SPIKA wa Bunge Mussa Azzan Zungu, ametoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kuchaguliwa kuwa Spika katika mkutano wa kwanza wa Bunge la 13 jijini Dodoma.
Katika hotuba yake, Spika Zungu ameshukuru Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan, kwa imani waliyomuonesha kwa kumteua kugombea nafasi ya uspika kwa tiketi ya CCM.
“Ninasimama kwa mara ya kwanza nikiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Namshukuru sana Mwenyekiti wa Chama changu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuniamini na kuchagua jina langu kugombea uspika wa CCM,” amesema.
Amesema kuwa licha ya wengi kuwania nafasi hiyo ndani ya chama, CCM iliamua kumpa dhamana hiyo kubwa, jambo analoliona kama heshima na wajibu wa kulitumikia Taifa kwa bidii.
Aidha, Spika Zungu amewashukuru wabunge wote waliompigia kura, akisema ushindi huo ni wa wabunge wote bila kujali itikadi zao.
“Nathamini sana kura na imani mlizonipa. Ushindi huu ni wetu sote. Naahidi kuwatumikia wabunge wote kwa usawa bila ubaguzi wowote. Ofisi ya Spika itakuwa wazi kwa kila mbunge,” amesema.
Pia amemshukuru Spika aliyemaliza muda wake, Dkt. Tulia Ackson, ambaye kwa sasa ni Rais wa Umoja wa Wabunge Duniani (IPU), kwa uongozi wake bora na mchango mkubwa alioutoa katika kuliongoza Bunge.
Spika Zungu ameahidi kushirikiana kwa karibu na Naibu Spika pamoja na Mwenyekiti wa Bunge katika kuhakikisha Bunge linafanya kazi zake kwa ufanisi, kuheshimu taratibu na kutoa maazimio yenye manufaa kwa wananchi.
“Tutahakikisha Bunge letu linaendelea kuwa chombo cha ushauri, usimamizi na uwakilishi wa kweli wa wananchi,” amesema.

