Simbachawene: Simu za mkononi zinaondoa umakini kwa watumishi wa umma
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema watumishi wengi wa umma wamepoteza umakini kutokana na kushika simu za mkononi ambazo zinawafanya wasahau majukumu yao kwa muda husika.
Simbachawene amesema hayo wakati akifunga semina ya Waajiri na Viongozi wa Matawi ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania ( TUGHE).
“Tunaenda nchi za wenzetu tunaona hawaingii na simu za mkononi ofisini, simu zinawekwa akitoka ndio anachukua na kufanya mawasiliano.
“Sisi watanzania matumizi ya simu yanatumika sivyo ofisini. Makundi yenyewe ni mengi. Kuna kundi la vikoba, la familia, ulilomaliza nao chuo, makundi chungu nzima. Kwa hali hii utahudumia watu saa ngapi?,” amehoji.
Anasema wapo watumishi wanaojitetea ni wafanyakazi wa kazi za ofisini, lakini na muuguzi naye ana makundi amemwekea mgonjwa drip, muuguzi huyo anaendelea kuchati.
Amesema likiwekwa katazo la matumizi ya simu za mkonono ofisini, mgogoro utakuwa ni mkubwa.
“Kama kuna kitu kinachoharibu afya zeru, ukishagusa simu ukitaka kulala usingizi unakata. Tumeathirika na simu, umakini wa kazi unapotea ukishika simu,”amesema.
Amesema watumishi wa umma wasipojikita kufanya kazi kwa bidii, kwa umakini nchi haitasonga mbele.
Kwa upande mwingine amesema watumishi wakitambua wao ni kioo cha jamii ni lazima wavae mavazi yanayokubalika kwa mujibu wa sheria.
Amesema isipowekwa sheria kali za watumishi wa umma,itakuwa kama maeneo mengine duniani.
“Watumishi wa umma baadhi yetu wanavaa vibaya hawajali kanuni za uvaaji. Tukumbuke sisi ni kioo cha jamii lazima uvae vazi linalokubalika kwa mujibu wa sheria.
“Nitamwelekeza Katibu Mkuu kutoa waraka maalum juu ya mavazi ya utumishi wa umma. Kwani huwezi mtumishi wa umma ukaacha bega wazi,” amesema.
Naye Katibu Mkuu Tughe, Hery Mkunda amesema lengo la semina ni kutoa uelewa wa pamoja kati ya waajiri na wafanyakazi sehemu za kazi.
Amesema hilo llitaboresha na kuondoa changamoto.