Na Lucy Ngowi
DODOMA: NAIBU Waziri wa Kilimo David Silinde amewataka wadau wa kilimo kushirikiana na serikali katika kuwarahisishia wakulima kufanya shughuli zao kisasa.
Silinde amesema hayo baada ya kugawa matrekta tisa kwa wakulima waliopatiwa mkopo wa vitendea kazi hivyo, alipotembelea banda la Agricom katika maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea Jijini Dodoma.
Pia amewataka wadau mbalimbali kuiga mfano wa taasisi ya Pass Leasing ambayo imetoa matrekta kwa wananchi tisa yatakayowarahisishia kilimo.
Katika banda hilo la Agricom ambapo wanufaika wa matrekta hayo walikuwa ni wanawake na vijana, Silinde amesema serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wadau hao wa kilimo kwa kuwa haiwezi kufanya kila kitu pasipo ushirikiano kama huo.
“Pass Leasing tunawashukuru kwa kazi mnayofainya ya kuwawezesha wananchi zana hizi za kilimo ,na hili ni jambo ambalo sisi kama serikali tutaendelea kuwaunga mkono. Tunahitaji wadau kama ninyi kuhakikisha hii sekta ya kilimo tunaisogeza pamoja.
“Na siku zote tumekuwa tukizungumza kwamba Sisi kama Wizara hatulimi,wanaolima ni wananchi na kilimo ni sayansi ambayo inahitaji ushirikiano wa pamoja ili kwenda mbele,kwa hiyo kwa kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ana dhamira ya dhati kuhakikisha kwamba kilimo tunakibadilisha kwenye viwango vingine,” amesema.
Amesema wizara hiyo imekusudia kutumia teknolojua za kisasa zitakazowarahisishia wakulima, kuachana na ulimaji wa jembe la mkono, lakini kufanya kilimo cha umwagiliaji pasipo kutegemea mvua kwa kujenga mabwawa ya umwagiliaji ili wananchi walime kwa tija.
Kwa upande wake Mkurugenzi Bodi ya Pass Leasing Rosebad Kurwijila amesema taasisi hiyo itawawezesha wakulima kupata zana za kilimo ili waweze kuzalisha kwa tija.
“Na tunapotoa vifaa hivi tunazingatia mnyororo wa thamani tangu kulima mpaka kuyaandaa mazao ,na mpaka sasa tumeshawawezesha wakulima 1,000.”amesema.
Baadhi ya wakulima waliokabidhiwa matrekta hayo wameishukuru PASS Leasing kwa kuwapatia mkopo huo ambao utawasaidia kuongeza tija kwa kulima kisasa na kuachana na jembe la mkono.