Na Lucy Ngowi
DODOMA: NAIBU Waziri wa Kilimo David Silinde amekabidhi nyaraka za kufungua masoko mapya kwa mazao ya kipaumbele tisa ili kuondoa vikwazo vya usafi mimea vinavyokwamisha usafirishaji wa mazao nje ya nchi.
Silinde amekabidhi nyaraka hizo katika hafla ya Uzinduzi wa Masoko wa Kufungua Masoko Mapya ya Mazao ya Kipaumbele kwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Salvatory Mbilinyi jijini Dodoma.
Ameyataja mazao hayo kuwa ni parachichi, ndizi, tumbaku, viazi mviringo, vanilla, nanasi, karafuu, pilipili manga na kakao.

Amesema amewasilisha nyaraka hizo za ufunguzi wa mazao kwa nchi ambazo fursa zake za masoko kwenye mazao hayo ya kipaumbele bado hazijafikia kutokana na uwepo wa masharti tangulizi ambayo yanapaswa kutimizwa kabla ya kuanza kusafirisha mazao.
“Hatua hii itawezesha kuondoa vikwazo vya usafi mimea kwa sasa vinakwamisha usafirishaji wa mazao hayo kwenye nchi lengwa.
“Hiki kinachofanyika leo ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba tunakuwa na masoko ya uhakika katika mazao yanayotokana na kilimo,” amesema.
Ametaja nchi hizo kuwa ni China inahitaji vanilla na nanasi, Indonesia karafuu, Singapore karafuu, Israeli parachichi, Malaysia parachichi, Canada pilipili manga.
Nchi nyingine ni Uturuki nanasi, Brazil nanasi, Marekani kakao, Afrika Kusini ndizi, Zambia viazi mviringo, Pakistan tumbaku na Iraki tumbaku.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru amesema taarifa ambazo nchi kwa kawaida huomba zinapopokea pendekezo la kufikia soko ni pamoja mimea iliyopendekezwa.
Pia Maeneo ya uzalishaji, wadudu wanaohusishwa na bidhaa iliyopendekezwa, usimamizi wa baada ya kuvuna na mpango wa sasa wa kuuza nje.
Amesema TPHPA inahakikisha kwamba hatua za ndani za usafi wa mazingira zinaoanishwa na viwango vya kimataifa kama vilivyowekwa na Mkataba wa Kimataifa wa Kulinda Mimea.
“TPHPA husaidia kuhakikisha kuwa bidhaa za kilimo za ndani zinaweza kushindana katika masoko ya kimataifa, na kuondoa vikwazo vya kiufundi katika biashara,” amesema.