Na Mwandishi Wetu
DODOMA: BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limesema kwamba anwani za Makazi zimerahisisha kutekeleza majukumu yake katika kutambua na kuwafikia wadau wake muhimu wa mazingira.
Kaimu Meneja wa NEMC Kanda ya Kati Novatus Mushi ameeleza hayo wakati Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa alipotembelea banda la NEMC katika Maonesho ya Wiki ya Anwani za Makazi yanayoendelea jijini Dodoma.

Mushi amesema anwani hizo za makazi zimerahisisha hasa kwenye shughuli za utoaji wa elimu na kufanya ukaguzi wa Mazingira kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo.
Vile vile imerahisisha katika kushughulikia malalamiko ya wananchi hususani changamoto ya sauti zinazozidi viwango, hivyo anwani za Makazi zimekuwa zikisaidia NEMC kufika kwa urahisi katika maeneo yanayolalamikiwa.

NEMC linashiriki Maonesho ya Wiki ya Anwani za Makazi yaliyozinduliwa rasmi na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa leo Februari sita, hadi Februari nane, 2025.