- Na Lucy Ngowi
TEKNOLOJIA za Akili Mnemba na Roboti zitasaidia kutatua changamoto mbalimbali nchini, kutokana na kuongeza ufanisi, kupunguza gharama, na kutoa ubunifu katika sekta mbalimbali.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la nane la Mwaka la TEHAMA Tanzania.
Silaa ametolea mfano changamoto hizo zinazoweza kutatuliwa na teknolojia hiyo ya akili mnemba na roboti kuwa ni afya, kilimo, elimu, na usimamizi wa rasilimali.
Amesema kama ilivyo kwa nchi nyingi zinazoendelea,
Tanzania inakabiliwa na changamoto kwenye jamii zinazohitaji suluhisho la haraka na endelevu.
Pia amesema katika wizara anayoiongoza, mbali na majukumu mengine anasimamia Sera ya Tehama 2016 ambayo imebainisha masuala ya Kisera, Kisheria na Taasisi katika kukuza matumizi ya Tehama Nchini.
Amesema kongamano hilo alilolifungua lina kauli mbiu isemayo, ‘Kutumia Uwezo wa Akili Mnemba na Robotiki kwa Mapinduzi ya Kiuchumi na Kijamii’, kwamba inafungua mjadala muhimu kwa wakati huu ambao dunia nzima inashuhudia mapinduzi ya kidijitali.
Awali amesema serikali imeendelea kuwekeza kwa kasi kubwa katika Tehama ambayo ndio nguzo kuu ya kufikia Uchumi wa Kidijitali.
“Dunia hivi sasa ipo katika kipindi cha Mapinduzi ya Nne, Tano na Sita ya viwanda ambapo shughuli za kiuchumi, kijamii na uzalishaji kwa kiasi kikubwa inakwenda kuendeshwa kwa kutumia teknolojia za juu za Tehama,” amesema.
Amesema kwa umuhimu huo Serikali imeendelea kuwekeza katika kufanya maboresho ya Kisera, Kisheria na Kitaasisi pamoja na kujenga uwezo kwa Watanzania ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa sehemu ya mabadiliko katika masuala ya Tehama duniani.
Silaa amesema katika sekta ya afya, Akili Mnemba na Roboti inaweza kusaidia kutoa utambuzi wa haraka wa magonjwa na kuboresha huduma za afya za msingi.
“Katika kilimo, Akili Mnemba na Roboti inaweza kuboresha tija kwa wakulima kwa kusaidia katika usimamizi bora wa uzalishaji na utafiti wa hali ya hewa.
“Pia, teknolojia hii inaweza kubadilisha kabisa jinsi tunavyoendesha biashara na utengenezaji wa bidhaa, kwa kuboresha mifumo ya usambazaji na kuongeza ufanisi,” amesema.
Amesema kwa kutumia Akili Mnemba na Roboti, viwanda nchini vinaweza kuongeza uzalishaji na kuwa na ushindani mkubwa kwenye soko la kimataifa.
“Akili Mnemba na Roboti inaweza kuimarisha mifumo ya elimu kwa kusaidia upatikanaji wa elimu bora kwa kila mwanafunzi, bila kujali eneo au hali yake ya kiuchumi.
“Kwa njia hii, tunaweza kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata fursa ya kujifunza na kuchangia katika maendeleo ya taifa letu,” amesema.