Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC), limetiliana saini na Kampuni ya CREGC & CREDC Mkataba wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa -SGR kutoka Uvinza Tanzania hadi Msongati Burundi.
Utiaji saini huo umeshuhudiwa na Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania Makame Mbarawa pamoja na Waziri wa Miundombinu, Ardhi na Makazi wa Burundi.
Akizungumza wakati wa utiaji saini huo, Waziri Mbarawa amesema thamani ya ujenzi huo ni Sh. Trilioni 5.6.
Mbarawa amesema mradi huo una vipande viwili ambavyo ni kutoka Uvinza mpaka Malagarasi, na kutoka Malagarasi hadi Msongati, jumla yake ikiwa ni Kilomita 282.

Waziri huyo ametoa maelekezo kwa TRC kuhakikisha mradi huo unafuata vigezo vya Kimataifa vya Usalama pia isimamie bajeti vizuri ili kuzuia gharama zisizokuwa za lazima.
Pia ameitaka TRC kushirikisha jamii mradi unaopita kwenye maeneo yao kwa kuwalipa fidia.
” Hakikisheni mnatoa fursa za ajira kwenye maeneo mradi unakopita,” amesema.
Naye Waziri wa miundombinu, Ardhi na Makazi nchini Burundi, Dieudonne Dukundane amesema uboreshaji wa huduma katika bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa reli hiyo ya kisasa, utainarisha uwekezaji sio kwa nchi hizo mbili tu, bali katika ukanda mzima.
Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba ameeleza kuwa fedha ya utekelezaji wa mradi huo ipo tayari, zilikuwa zinasubiri mjenzi apatikane.

“Reli ili iwe na tija ni lazima yote iwe imekamilika. Nitoe uhakika kwamba fedha kwa ajili ya vipengele vingine inakamilishwa. Ipo katika hatua za mwisho,” amesema.
Awali Mkurugenzi Mkuu TRC, Masanja Kadogosa ameshukuru utiaji saini huo wa kipande cha saba na cha nane ikiwa ni awamu ya pili ya mwendelezo wa reli ya kisasa.

Amesema ujenzi huo utachukua miezi 72, ukijumlisha kilomita 282, kilomita 240 zitakuwa za njia kuu na 42, njia za kupishana.

“Tutaendelea kusimamia kutimiza lengo la ujenzi unaotekeleza kwa viwango vilivyokusudiwa,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso ameshauri kipande kutoka Dodoma – Makutupora kwenda Tabora hadi Kigoma, kiende sambamba na ujenzi huo unaoanza.