Na Lucy Ngowi
MBEYA: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imechukua hatua madhubuti kuimarisha ustahimilivu wa Taifa dhidi ya majanga kwa kutekeleza sera, sheria na miradi inayolenga kulinda maisha, mali na rasilimali za nchi.
Akizungumza jijini Mbeya katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa, Majaliwa amesema hatua hizo ni pamoja na kuhuisha Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa (2025), Mkakati wa Taifa (2022–2027), na Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa (2022).

Ameeleza kuwa Serikali imefanikiwa kuongeza usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kupitia TMA hadi asilimia 85, hali ambayo imepunguza madhara ya maafa kwa zaidi ya asilimia 30. Pia, mifumo ya tahadhari ya mapema imeimarishwa kupitia teknolojia na Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa Majanga.
Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa Bwawa la Kidunda (Tsh bilioni 329), Bwawa la Farkwa (Tsh bilioni 312), na Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria hadi Simiyu (Tsh bilioni 440).

Sekta ya kilimo pia imenufaika kupitia mbinu za kilimo himilivu kama umwagiliaji, matumizi ya mbegu bora, pamoja na mifumo ya tahadhari mapema ili kuwasaidia wakulima kukabiliana na majanga ya asili.
Waziri Mkuu amesema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeboreshwa kwa vifaa, teknolojia na mafunzo ya kisasa, jambo litakalowezesha uokozi wa haraka wakati wa majanga.
Ametoa wito kwa sekta binafsi kuwekeza kwenye miradi yenye mwelekeo wa ustahimilivu, ikiwemo uwekaji wa bima na kufuata miongozo ya serikali ili kuwalinda wananchi na mali zao.

Kwa upande wake, Waziri William Lukuvi na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, Sandra Hakim, wamehimiza ushiriki wa wadau wote katika usimamizi wa maafa, wakiwemo vijana, viongozi wa jamii, na taasisi za kimataifa katika kuzuia, kujiandaa na kurejesha hali baada ya majanga.