Na Lucy Ngowi
MBEYA: SERIKALI imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha vijana wanapata fursa sawa za kujiletea maendeleo na kuchangia kikamilifu katika ustawi wa taifa, kupitia utekelezaji wa sera, sheria, na mikakati madhubuti ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza Jijini Mbeya wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Vijana la Tanzania, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mary Maganga, amesema serikali imeweka mifumo ya kitaasisi, mipango kazi, na miongozo yenye lengo la kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana nchini.

Kongamano hilo la siku mbili linalofanyika katika Ukumbi wa City Park Garden, linaendelea kesho Oktoba 13, 2025, likiwa limekusanya zaidi ya vijana 1,500 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na Maofisa Vijana kutoka Halmashauri zote.
Maganga amesema lengo kuu la kongamano hilo ni kuwawezesha vijana kujenga uwezo wa kushiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, kukuza ushirikiano, pamoja na kubadilishana mawazo, uzoefu na mbinu za kuleta maendeleo.
“Vijana ni nguvu ya mabadiliko na maendeleo katika jamii zetu. Ni lazima tutumie vema nguvu hii kubadilisha dunia kuwa mahali bora kwa ajili ya wote,” amesema.
Aidha, amewataka vijana kutumia jukwaa hilo kujadili changamoto zinazowakabili, ili serikali iweze kuyachukua maoni yao na kuyatumia katika maboresho ya sera, sheria na miongozo kwa manufaa ya vijana wote nchini.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amewahimiza vijana kote nchini kushiriki kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, kwa kuwachagua viongozi wanaoendana na ndoto, malengo na matumaini ya taifa.
Mapema, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Rodrick Mpogolo, amewahimiza vijana kuwa wazalendo, kuipenda nchi na kujivunia taifa lao, akisisitiza kuwa kila kijana ana mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Seleman Mvunye, ameeleza kuwa kongamano hilo limehusisha vijana kutoka kila kona ya nchi, lengo likiwa ni kuhakikisha sauti zao zinasikika na mchango wao unatambulika katika ujenzi wa taifa.