Na Lucy Lyatuu
SERIKALI imeahidi kuwasiliana na mamlaka husika ili kukipatia dawa kilio cha ushuru kwa wamiliki wa malori wadogo na wa kati Tanzania ili kupunguza malalamiko.
Hayo yamesema leo Dar es Salaam na Meneja wa Usalama kutoka Mamlaka Ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof Godius Kahyarara
Amesema hayo katika mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha wamiliki wa malori wadogo na wa k ati Tanzania (TAMSTOA).
Amesema serikali inaendelea kufanikisha kutatua changamoto za usafirishaji zinapojitokeza na kwamba inawahakikishia sekta hiyo inakuwa imara na kuboresha mazingira wezeshi katika kukuza uchumi wan chi.
Amesema kuhusu hatua za ujenzi wa reli ya kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda Kwala kupeleka shehena za ujenzi ziko katika hatua nzuri na serikali inajipanga kuanza kutekeleza mara moja.
Aidha amesema serikali ipo katika hatua mbalimbali kuhakikisha upanuzi wa barabara ya Morogoro hadi Chalinze unafanyika kwa mfumo wa ushirikiano wa sekta binafsi na umma.
Amesema inafanya hivyo kwa kuwa maendeleo yote duniani yamefanyika kwa njia shirikishi.
Amesema pia serikali ipo katika hatua mbalimbali za upanuzi wa barabara ya Mbozi hadi Tunduma ambayo kwa sasa inaonekana kuwa finyu huku magari ya mizigo yakiongezeka kwa kiasi kikubwa.
Kadhalika amesema changamoto na tofauti katika mizani hasa kutoka eneo la Mpemba,Makambako na Iringa, serikali inafanyia kazi na mabadiliko yataonekana siku chache zijazo.
Vilevile amesema Wizara itawasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuona namna nzuri ya kuondoa malalamiko ya wao kukamatwakamatwa haswa eneo la Mikumi Morogoro.
Aidha amesema Serikali inapinga vikali vitendo vya rushwa, hivyo inaahidi kufuatilia askari wa usalama barabarani wanaoendeleza na kwamba haitomvumilia yoyote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAMSTOA, Chuki Shaban amesema yapo Malori 26,000 yakitoa ajira 52 ,000 na kuiomba serikali kuwa na mazingira rafiki ya sekta ya usafirishaji.
Amesema malori hayo husafirisha mizigo yapatayo 192,996 na magari hayo hutumia mafuta lita milioni 62.4 yakinunuliwa kwa sh milioni 187 kwa siku,hivyo ni sekta yenye mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi.
Aidha wameiomba serikali kupanua barabara inayoanzia bandarini Dar es Salaam hadi Chalinze mkowa wa Pwani kwa kuwa ni nyembamba yenye kuongeza msongamano barabarani.
“Ni wakati sasa serikali kuona umuhimu wa kutafuta barabara nyingine za pembezoni hata kama nimza vumbi ziweze kutumika ili kundoa msongamano,” amesema Shaban