Na Lucy Ngowi
GEITA: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema sekta ya madini inaendelea kuwa mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi nchini, baada ya kufanikisha ukuaji wa asilimia 10.9 mwaka 2022 na kuchangia asilimia 10.1 kwenye Pato la Taifa mwaka 2024, kutoka asilimia 9.0 mwaka uliopita.
Majaliwa allmesema hayo kwenye uzinduzi wa Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.
Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, hasa katika kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato, udhibiti wa biashara ya madini na matumizi ya teknolojia kama mfumo wa online mining cadastre, pamoja na kuanzishwa kwa masoko ya madini na ufuatiliaji wa mikataba ya uwekezaji.

“Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta hii ili kuhakikisha madini yanachangia maendeleo ya kiuchumi kwa Watanzania wote,” amesema Majaliwa.
Ametoa wito kwa wadau wa sekta ya madini kuwekeza zaidi kwenye teknolojia ili kuongeza tija katika shughuli za utafiti, uchimbaji, usafishaji na biashara ya madini.
“Teknolojia ni msingi wa maendeleo ya sekta hii. Bila teknolojia, hatuwezi kuongeza tija, kulinda mazingira, wala kuhakikisha usalama wa wachimbaji,” amesema.
Akizungumzia mafanikio ya wachimbaji, Majaliwa amesema kuwa kati ya mwaka 2021 hadi 2025, wachimbaji wadogo mkoani Geita wamezalisha zaidi ya kilo 22,000 za dhahabu zenye thamani ya Sh. trilioni 3.44, huku Serikali ikivuna Sh. bilioni 235.5 kupitia mrabaha.
Kwa upande wa makampuni makubwa, Geita Gold Mine na Buckreef wamezalisha jumla ya kilo 76,530 za dhahabu zenye thamani ya Sh. trilioni 11.38 na kuipatia Serikali zaidi ya Sh. bilioni 793 kama mrabaha.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahya Samamba, ameongeza kuwa Tanzania sasa ina viwanda vya kuzalisha vifaa vya uchimbaji, na kwamba katika mwaka wa fedha 2024/2025 uzalishaji wa dhahabu umefikia tani 62 kiwango kinachoiweka Tanzania miongoni mwa wazalishaji watano bora wa dhahabu barani Afrika.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amesema Serikali imefanya kazi kubwa ya kusambaza umeme vijijini, hususan katika maeneo ya wachimbaji wadogo, ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
“Tumehakikisha maeneo mengi ya wachimbaji wadogo yamefikishiwa umeme, kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Shigela.