Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kitakachofanyika mkoani Arusha.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amesema hayo alipozungumza na Waandishi wa Habari kuhusu uelekeo wa maadhimisho hayo.
Gwajima amesema kama taifa linayo mengi ya kujivunia ambayo ni kielelezo cha utashi na uthubutu wa Rais Samia katika kukuza usawa na uwezeshaji wanawake nchini.

” Serikali kwa kutambua umuhimu wa siku hii inahimiza wanawake na wananchi kwa ujumla kujitokeza katika maadhimisho kwa kushiriki matukio yote kuanzia uzinduzi, maonesho na makongamano ili kuwa na maadhimisho yenye tija na mafanikio kwa ustawi na maendeleo ya wanawake hapa nchini,” amesema.
Amesema kauli ya mwaka huu ni ‘Wanawake na Wasichana 2025’ inalenga kuhamasisha jamii katika kukuza usawa, haki na uwezeshaji wa wanawake na wasichana na kwa kuzingatia kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Amesema lengo la kaulimbiu ni kuwafanya wanawake na wasichana wajiamini, wajiandae na wajitokeze kugombea fursa za uongozi.

Amesema katika kuadhimisha siku hii, serikali imeunda kamati ya Kitaifa ya maandalizi ya maadhimisho hayo kwa lengo la kuhakikisha yanabeba sura ya kitaifa na kushirikisha wadau wote.
Amesema Machi mosi, 2025 uzinduzi utafanyika katika mikoa, wilaya na Kata zote nchini.
Machi tatu hadi sita mwaka huu 2025, kutafanyika makongamano ya Kikanda katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Geita, Mbeya, Lindi na Kigoma.
Amesema Machi tano mpaka nane, 2025 kutakuwa na maonesho ya wanawake wajasiriamali, taasisi za umma na binafsi na makampuni jijini Arusha.
Na Machi nane, mwaka huu itakuwa kikele cha maadhimisho hayo.