Na Danson Kaijage.
RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika siku ya maadhimisho ya Mashujaa kitaifa itakayofanyika kesho Julai 25, mwaka huu 2025 Jijni Dodoma.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Doto Biteko amesema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari.

Biteko amesema kila mwaka Julai 25 kunakuwa na maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa ambayo itafanyika katika Uwanja na Mnara wa Mashujaa uliopo Mji wa Serikali, Mtumba Dodoma.
“Mgeni Rasmi katika tukio hili anatarajiwa kuwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Siku hii ni maalum kwa ajili ya kuwakumbuka, kuwaenzi, na kuwaheshimu mashujaa wetu waliotoa maisha yao, nguvu zao, na sadaka zao kwa ajili ya uhuru, amani, na maendeleo ya Taifa letu,” amesema.

Amesema Taifa linawakumbuka mashujaa waliopoteza maisha yao katika uwanja wa vita, waliostaafu baada ya kulitumikia Taifa kwa uaminifu, na wale waliopata majeraha katika kuilinda nchi.
Ameeleza kuwa kutokana na heshima hiyo, saa sita usiku wa Julai 24, 2025 Mwenge wa Kumbukumbu ya Mashujaa utawashwa rasmi na mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, kwa niaba ya Rais kuashiria kuanza kwa maombolezo ya Mashujaa hao.
“Katika siku ya maadhimisho yaani Jula8 25, 2025 kuanzia saa tatu asubuhi kutakuwa na gwaride rasmi la heshima litakalofanywa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama,” amesema.