Na Danson Kaijage
DODOMA: RAIS Samia Suluhu Hassan amesema hakuna sheria inayomkataza mwanamke kumiliki ardhi kwani naye ana haki kama ilivyo kwa mtu yoyote yule kwa kuzingatia taratibu za nchi.
Samia ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Sera ya Taifa ardhi ya mwaka 1995 toleo la mwaka 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
Amesema kuwa mwanamke naye ana haki ya kumiliki ardhi kwa kufuata misingi na taratibu na sheria za nchi kama alivyo mtu mwingine yoyote ilimradi awe ni mtanzania.
Katika hatua nyingine amewataka watendaji katika Wizara husika kuhakikisha wanapima ardhi na kuwamilikisha wananchi kwa kulipia gharama kwa mujibu wa sheria ya nchi.
Amesema kuwa wapo watu ambao siyo waaminifu ambao wanashirikiana na watu wa ardhi kwa kufuta hati za watu na kuwapora ardhi zao na kuwapa watu wengine jambo ambalo halipendezi wala halikubaliki.
Amesema ardhi itaendelea kuwa mali ya Umma huku msimamizi mkubwa akiwa Rais na ardhi itakodishwa wenyeji na kuhakikisha mipaka inatambuliwa vyema .
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Deogratius Ndejembi amehimiza utekelezaji wa sera hiyo na kusema kuwa ni kati ya sera ambayo itakuwa mlinzi wa matumizi ya ardhi.
Amesema Wizara ya Ardhi na Tawala za Mikoa na Ofisi ya Rais -Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana watahakikisha wanapima ardhi na kubaini nchi ina ukubwa gani na kutambua matumizi bora ya ardhi kwa faida ya vizazi vijavyo.
“Tunatambua kuwa tangu kuwe kwa mipaka ya nchi ardhi haiongezeki lakini watu wanaongezeka hivyo Wizara ina kila jukumu la kupima kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinapimwa na kupangiwa matumizi bora ili kuweka utaratibu mzuri wa kurithisha vizazi vijavyo, amesema. .