Na Lucy Lyatuu
RIPOTI ya Utafiti kuhusu waendesha pikipiki na bajaj nchini imebaini kuwepo kwa vikwazo katika kazi hiyo huku wanawake wakikabiliwa na ukatili wa kijinsia pamoja na kutengwa
Aidha imeelezwa kuwa kazi hiyo bado ni hatarishi licha ya kuwa fursa kubwa ya kujipatia kipato katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa katika uzinduzi wa ripoti kupitia Utafiti uliofanywa na Chama Cha Wafanyakazi Wa Mawasiliano Na Usafirishaji Tanzania (COTWU-T) na Shirila La Friedrich Ebert Stiffung(FES) Tanzania .
Utafiti huo umefanywa katika mkoa Wa Dar es Salaam katika wilaya ya Kinondoni, Temeke, Ubungo na Ilala na Michaela Collord na Nice Mwansasu ukijumuisha madereva 150 Wa bodaboda wakiwemo wanawake 47.
Akizungumza Nice amesema ripoti hiyo imeangazia changamoto za kimuundo na fursa zilizopo ndani ya sekta hiyo kwa kuzingatia hasa usafiri ni suala endelevu,Maisha salama na Changamoto zinazowakabili madereva wanawake.
Amesema asilimia 68 ya madereva wa kiume na asilimia 78 ya madereva wa kike wameripoti kuongezeka kwa kipato baada ya kujiunga na kazi hiyo na kuweza kuhudumia watu takriban wanne hadi watano.
Amesema kazi hiyo bado ni hatarishi ikiwa na vikwazo kadha wa kadha ikiwemo urasimu, siasa na ukosefu wa mshikamano kati ya vyama vya madereva.
Amesema pia yapo madhara kwa watoa huduma hizo hususani wale wa mtandao ambapo mara nyingi hupunguziwa kipato chao.
Nice amesema ipo haja ya kushirikisha madereva latika miradi ya barabara, kuwe na sehemu za kupumzikia na upangaji wa miji kwa muda mrefu ili kuepuka kuondoakundi hilo katika maeneo yao ya kazi.
Kuhusu madereva wa kike amesema kuna haja yakutolewa mafunzo kuhusu namna yakupambana na ukatili wa kijinsia na kampuni za mabasi zikihamasishwa kuajiri wanawake kwa kuwa ni kundi linaloweza.