Na Lucy Ngowi
DODOMA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, amezindua rasmi miongozo mitatu na mifumo miwili ya kielektroniki yenye lengo la kuboresha uratibu, usimamizi na utoaji wa huduma katika sekta za kazi, ajira, vijana na watu wenye ulemavu.

Uzinduzi huo umefanyika leo Agosti 22, mwaka 2025 jijini Dodoma, ambapo Waziri Ridhiwani amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha huduma kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Amesema miongozo na mifumo hiyo inalenga kujenga msingi wa majadiliano jumuishi na yenye tija baina ya wadau wa kazi, pamoja na kuimarisha usimamizi wa mawakala wa ajira, kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinalindwa, na kuwezesha ukusanyaji wa taarifa sahihi za soko la ajira kwa kutumia mifumo ya kidijitali.
Miongozo iliyozinduliwa ni pamoja na Mwongozo wa Majadiliano baina ya Serikali, Vyama vya Wafanyakazi na Vyama vya Waajiri wa mwaka 2025, Mwongozo wa Uratibu wa Vyama vya Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2025, pamoja na Mwongozo wa Wakala Binafsi wa Ajira wa mwaka 2025.

Pia mifumo ya kielektroniki iliyozinduliwa ni Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Soko la Ajira wa mwaka 2025 na Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri ya Usuluhishi na Uamuzi wa mwaka 2025.
Waziri Ridhiwani amesema mifumo hiyo itawezesha utatuzi wa mashauri ya kazi kwa haraka, kuongeza uwazi, na kusaidia wananchi hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya taifa.

Ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau mbalimbali kwa ushirikiano wao katika maandalizi ya miongozo na mifumo hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mary Maganga amesema uandaaji wa miongozo hiyo ulikuwa wa kushirikisha wadau mbalimbali.
Ambao ni Shirika la Kazi Duniani (ILO), Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), pamoja na Chama cha Mawakala Binafsi wa Ajira (TRAA).
Kwa upande wake, mwakilishi wa Katibu Mkuu Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Rashid Mtima amesema wafanyakazi wana imani kubwa na serikali kutokana na hatua ya kupandisha mishahara kwa asilimia 35 mwaka huu, hatua ambayo imeongeza ari kwa wafanyakazi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Patricia Shao amesema chama hicho kitaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa sekta ya ajira kuhakikisha Tanzania inakuwa na nguvu kazi bora na yenye tija.
Amesema kuwa miongozo hiyo inalenga kufanikisha lengo hilo.