Na Mwandishi Wetu
KILIMANJARO: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema Mwenge wa Uhuru umepelekwa juu ya Mlima Kilimanjaro baada ya kuhitimisha mbio kwa siku 195.
Ridhiwani amesema hayo ikiwa ni agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kwamba mwaka huu 2024, mwenge huo baada ya kuhitimisha mbio zake upelekwe katika mlima huo.
Amesema kitendo cha kupeleka mwenge huo juu ya mlima Kilimanjaro kinaitangazia dunia kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni imara, na kwamba Tanzania itaendelea kulinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Ridhiwani amesema hayo katika hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro wakati wa hafla ya kupokea kikosi maalumu cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambacho kimepewa jukumu la kupeleka Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Taifa la Tanzania kilele cha mlima Kilimanjaro.
Pia Ridhiwani amehamasisha vijana kuendelea kuenzi falsafa za mwenge wa uhuru ulioasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961.
Awali akizungumza, Waziri wa Maliasili na Utalii, Pindi Chana amesema kupandishwa mwenge wa uhuru Mlima Kilimanjaro mwaka huu 2024 kunaleta hamasa ya uzalendo kwa wananchi hususan wakati huu ambao Tanzania inaadhimisha miaka 60 ya uhuru na mafanikio ya Taifa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amemshukuru Rais Samia kwa kuridhia mwenge wa uhuru kupandishwa kwa mara nyingine katika kilele cha mlima Kilimanjaro.
Kwa upande wake, Kiongozi wa kikosi hicho Maalum, Luteni Kanali Khalid amemhakikishia Waziri Ridhiwani kuwa kikosi hicho kinaufikisha, kinaulinda na kuutunza Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Taifa la Tanzania hadi katika kilele cha mlima Kilimanjaro.