Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema hatua ya Halmashauri ya Tunduma kutoa mikopo yenye thamani ya Sh. Bilioni 4.6 kwa vikundi 150, ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyeelekeza Halmashauri kuanza kutoa mikopo hiyo
Rais Samia ameelekeza mikopo hiyo kutolewa kwa kutumia mfumo mpya wa utoaji na usimamizi.

Akizungumza wakati akikagua miradi ya maendeleo mkoani Songwe, Ridhiwani amesema baada ya Rais Samia kuelekeza uboreshaji wa mikopo hiyo, dirisha la utoaji mikopo lilifunguliwa rasmi Septemba 2024.
Pia amesema serikali imejitahidi kufungua fursa kwa vijana na kuwezeshwa mikopo kupitia vikundi.
Ameshauri vikundi kutumia fedha za mikopo kwenye miradi yenye tija na kurejesha kwa wakati ili na wengine wanufaike na mikopo hiyo.
Vile vile Waziri huyo amekagua na kuweka jiwe la msingi katika miradi ya Ujenzi wa majengo ya Hospitali ya Halmashauri ya Momba, Jengo la NMB na Majengo ya madarasa ya ghorofa ya shule ya sekondari Uwanjani na kikundi cha Vijana cha Ufugaji kuku Chipaka.
Amewapongeza Wabunge wa majimbo hayo ya Momba na Tunduma, Condester Sichwale na David Silinde kwa kuhakikisha wanatafsiri maono ya. Rais Samia kwa vitendo ya kuwaletea maendeleo wananchi
Naye Mkuu wa mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika mkoa huo hali inayo chochea mapato ambayo husaidia Halmashauri za mkoa huo.