Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA), umetoa jumla ya majiko banifu 10,650 mkoani Pwani ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za Serikali za kuhakikisha kila mwananchi anatumia nishati safi ya kupikia nchini.
Akizungumza leo Agosti 18, 2025 ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Meneja wa Teknolojia za Nishati kutoka REA, Michael Kyessi amesema mradi huo unalenga kuuza na kusambaza Majiko Banifu kwa bei ya ruzuku ambapo mwananchi atachangia asilimia 20 ya gharama ya jiko huku asilimia 80 zikitolewa na Serikali.

“Mwananchi wa kawaida atachangia asilimia ishirini tu za gharama za jiko ambapo bei ya jiko ni sh 56,000 na mwananchi atagharamika kuchangia shilingi 11,200 tu baada ya ruzuku kutolewa na Serikali” amesema Kyessi.
Pamoja na hilo Kyessi amebainisha thamani ya mradi huo kwa ujumla ni sh milioni 596,400,00 ambapo Serikali kupitia REA imetoa ruzuku ya sh milioni 477,120,00 ambayo ni sawa na asilimia 80.
Katika hatua nyingine, REA inatekeleza lengo la Serikali ya Tanzania kufikia mpango wa Umoja wa Mataifa wa “Nishati Endelevu kwa Wote” (SE4ALL) wa upatikanaji wa nishati
kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.

Mradi huo utatumia nishati Jadidifu ili kuweza kufikia wananchi wa maeneo ya visiwani na utekelezaji wake ni kwa kupitia mradi wa Ufadhili unaotegemea Matokeo (RBF) kupitia Benki ya Dunia.
“Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kufunga mifumo ya umeme jua maeneo ya visiwani kwa kutoa ruzuku kwa bei ya mwisho ya mtumiaji wa mfumo wa Umeme Jua ili kufanikisha upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo yaliyo mbali na Gridi ya Taifa, ” Amesema Kyessi.
Kyessi amesema katika Mkoa wa Pwani mradi wa umeme jua unategemea kuhudumia visiwa 13 na jumla ya watoa huduma wawili wanategemea kuhudumia visiwa hivyo kupeleka jumla ya mifumo 2,243 ndani ya kipindi cha miaka miwili na gharama za mradi kwa mkoa wa Pwani ni sh bilioni 1.372 ambapo ruzuku ni milioni 935.7 sawa na asilimia 69 ya gharama zote ya mradi na sh milioni 436.6 ni fedha kutoka kwa wanufaika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameipongeza REA kwa mkakati wa kuendelea kuongeza matumizi ya Nishati safi na kuondoa kero kwa wananchi kuhusu matumizi ya kuni na mkaa ambayo ni hatarishi kwa afya zao.
Mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miezi 15 katika mkoa wa Pwani na jumla ya Majiko Banifu 10,650 yatasambazwa kwa wananchi.