Na Lucy Lyatuu, Singida
CHAMA cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), kimetangazwa rasmi kuwa mwanachama wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Taarifa hiyo ya kufurahisha kwa JOWUTA imetolewa na Katibu Mkuu wa TUCTA, Henry Nkunda, wakati akisoma risala ya wafanyakazi mbele ya Rais Samia, kwenye maadhimisho ya sherehe za Mei mosi Kitaifa zilizofanyika kwenye Viwanja vya Bombadia mjini Singida leo.
Nkunda amesema pamoja na JOWUTA vyama vingine ambavyo vilivyopokelewa kama wanachama wapya ni Chama cha Wafanyakazi wa Kampuni Binafsi za Ulinzi nchini (TUPSE) na Chama cha Wafanyakazi za Huduma za Viwandani Tanzania (TASIWU).
Baada ya vyama hivyo vitatu kuwa mwanachama rasmi wa TUCTA sasa itakuwa na jumla ya vyama vya wafanyakazi wanachama 16.
“Mheshimiwa Rais TUCTA ilipokea maombi ya vyama tisa vya wafanyakazi ambapo baada ya Bazara Kuu kukutana na kujadili vyama vitatu vya JOWUTA, TUPSE na TASIWU vimefanikiwa kukidhi vigezo na kujiunga na shirikisho hili, bado tunaendelea na mchakato wa kuunga vyama vingine , lengo letu ni kuwa wamoja,” amesema.
Akizungumza mjini hapa na viongozi wa JOWUTA ,Rais wa TUCTA Tumaini Nyamuhokya amepongeza JOWUTA na vyama vingine kudumisha ushirikiano na kufanya kazi na shirikisho kwa maslahi ya wanachama.
“Mimi muda mrefu nilikuwa napenda JOWUTA mkamilishe taratibu na kuwa wanachama wa TUCTA ili tusaidiane kusaidia tasnia yenu”amesema
Mwenyekiti wa Taifa wa JOWUTA, Mussa Juma amemweleza Rais huyo wa TUCTA kuwa JOWUTA imepokea kwa furaha kubwa tangazo la kukubaliwa kuwa mwanachama wa shirikisho.
Amesema JOWUTA itajitahidi kufuata taratibu na Kanuni za TUCTA, ili kuwa mwanachama hai na hivyo kushirikiana kutatua changamoto katika tasnia ya habari nchini.
“Tunashuru sana kukubaliwa maombi yetu ya muda mrefu kuwa mwanachama wa TUCTA na sasa tunaimani kwa kutumia uzoefu wa TUCTA katika kushughulika na masuala ya kazi, ili wafanyakazi wa vyombo vya habari wanufaike”amesema
Naye Katibu wa JOWUTA Selemani Msuya amesema chama hicho kukubaliwa kujiunga TUCTA ni ushahidi tosha kwamba linapambania maslahi ya wanachama wake na kuwataka wanachama wake walipe ada kwa wakati ili kujenga ushirikiano huo.
“Hii ni habari njema kwetu sisi JOWUTA, napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wanachama walipe ada kwa wakati na waandishi wengine wajiunge ili kuwa na nguvu pamoja katika kupigania maslahi yetu,” amesema.