Na Lucy Ngowi
PWANI: RAIS Samia Suluhu Hassan ameridhia malipo ya Sh. Milioni 800 kwa wananchi 429 wa Kata ya Mkange wanaopisha ujenzi wa Barabara ya Afrika Mashariki inayojengwa toka Tanga kupita Kata hiyo hadi Makurunge Bagamoyo.
Mbunge wa Jimbo la Chalinze ambaye pia ni Waziri Wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana,Ajira na wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema hayo wakati wa mkutano aliofanya na wananchi wa vijiji vitano.
Katika mkutano huo, Ridhiwani ameishukuru serikali kwa kuendelea kutatua kero za wananchi, pia amemshukuru Rais Samia kwa kuridhia fedha hizo zilipwe ili wananchi wapishe na kupata maendeleo.

Vile vile ameishukuru serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya barabara mbalimbali katika halmashauri hiyo zitakazoongeza tija kiuchumi kwa wananchi wanaopitiwa na miundombinu hiyo.
Pia Ridhiwani ameishukuru serikali kwa matayarisho ya ujenzi wa barabara toka Mandera hadi Saadan ambayo inakwenda kufungua fursa kiuchumi.
Wakizungumza baada ya mkutano huo wananchi wa Mkange, wameeleza furaha yao na kumshukuru Mbunge wao Ridhiwani ambaye siku zote amekuwa akipambana kuhakikisha anatatua changamoto zao.

Sheikh wa Mkange, Alhaj Khamis Nassor, ameelezea kuridhishwa namna mbunge wa jimbo hilo anavyoshughulika na changamoto za wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi, Mwenyekiti wa Chama hicho Mwidadi Mauya amesema amepokea taarifa hiyo kwa furaha kubwa, akisema hivi sasa atakwenda kukisimamia chama kwakuwa jambo hilo lilimnyima uhuru wa kuzungumza.
”Mbunge huyu ni wa mfano wa kuigwa kwa jinsi anavyopigania maendeleo ya watu hasa watu wa Mkange. Sisi tutamuunga mkono na tuko naye na Mheshimiwa Rais ametuheshimisha Chama Cha Mapinduzi.
” Hakuna shida mwaka huu tutashinda kwa ukubwa sana,” amesema.
Serikali imeendelea kutenga fedha za maendeleo katika halmshauri hiyo, kwani zaidi ya Sh.Bilion 130 za miradi mbalimbali zimepelekwa wilayani hapo zikiwemo fedha za Elimu, Maji na Barabara.