Na Mwandishi wetu Zanzibar
ZANZIBAR: RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hussein Ali Mwinyi amezindua Ripoti ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Zanzibar.
Uzinduzi huo umefanyika kwa ushirikiano kati ya Wataalamu kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Wataalamu kutoka Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar (WMNMZ).
Akizindua ripoti hiyo, Mwinyi amewapongeza wataalamu hao kwa kazi nzuri iliyofanyika ya kubainisha aina ya madini na mahali yaliyopo visiwani humo.

Amesema ripoti hiyo ya Jiolojia itatumika kwenye sekta mtambuka zikiwemo madini, nishati,maji, ujenzi, kilimo, elimu, afya na utalii ambazo ni muhimu katika ustawi wa jamii na uchumi wa Zanzibar.
Katikq uzinduzi huo, Rais Mwinyi ameitaka Wizara ya Maji, Nishati na Madini ya Zanzibar kuhakikisha inaisambaza ripoti hiyo kwa taasisi zote zinazoguswa na tafiti hizo ili kuifanyia kazi kwa manufaa ya Taifa na kuongeza tija kwenye uchumi wa nchi.
Pia Rais Mwinyi ameitaka Wizara ya Madini kupitia taasisi ya GST kudumisha mashirikiano yaliyopo katika Sekta ya Madini na kusisitiza kuendelea kufanya tafiti mbalimbali kwa lengo la kuendelea kugundua maeneo mapya yenye viashiria vya madini, fursa za utalii na maeneo yenye majanga ya asili nchini.

Pamoja na mambo mengine, Rais Mwinyi ametoa Vyeti kwa wataalamu walioshiriki kufanya tafiti na kuandaa ripoti hiyo kama pongezi na kumbukumbu kwa wataalamu hao.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema utafiti uliyofanyika visiwani Zanzibar utawezesha uimarikaji wa uchumi katika visiwa hivyo na kubadilisha maisha ya watanzania wanaoishi visiwani humo.
Waziri Mavunde amesema matarajio ya matokeo ya utafiti huo yatatumika kuvutia uwekezaji mkubwa na kuchochea uchumi wa Taifa.
Naye, Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar Shaibu Kaduara amesema utafiti uliofanyika katika visiwa hivyo ni utafiti wa awali utakaohitaji kufanyika kwa utafiti wa kina ili kubaini kiwango cha Madini yaliyopo visiwani humo.
Awali, Mkurugenzi Idara ya Nishati na Madini, Said Mdungi amesema Zanzibar kuna Jiolojia ya miamba tabaka ambapo alitaja aina za hiyo miamba, udongo na viashiria vya miamba yenye maji.
Kwa upande wa madini amesema miongoni mwao ni madini tembo, madini ujenzi, chokaa na silica.