Na Lucy Lyatuu
RAIS Dkt Samia Suluhu Hassan amewaapisha mawaziri wapya na kuwataka kujitahidi kutumia rasilimali za ndani ya nchi ili kupata fedha za kutekeleza miradi.
Amesema serikali itahakikisha itafanya miradi yote wenyewe, hatutasubiri vyanzo vingine vya nje kama vile mikopo, kama ikija itawakuta wanaendelea na kazi.
Rais Samia amesema hay oleo Dodoma wakati akiapisha mawaziri wapya na kuwataka kuhakikisha kuwa majukumu waliyopeana na viapo walivyoapa ni kwamba wamekubali kuwatumikia watu, na kauli yao iwe ni Kazi na Utu, hivyo utu uanze na wao kwa kuonesha utu kwa wengine kwa kuwatumikia vema.
Amesema kazi yao kuu ni kuwajibika kwa wananchi na nchi kwa ujumla, wakatekeleze yale yote waliyoahidi kwa wananchi,na kukumbuka kwamba muda walionao ni mchache na mambo ni mengi.
“Tujitahidi kutumia rasilimali zetu za humu ndani ili tupate fedha za kutekeleza miradi yetu, tutahakikisha tunafanya miradi yetu yote wenyewe, hatutasubiri vyanzo vingine vya nje kama vile mikopo, kama ikija itatukuta tunaendelea na kazi,” amesema.
Amesema ndani ya siku 100 watekeleze na kukamilisha kazi zote walizoahidi kutimiza ndani ya siku hizo na kwamba wakionesha matokeo kwa wananchi na siyo ofisini.
Rais Samia amewataka wasiubebe uwaziri kama fahari, bali wafanye kazi kwa maslahi ya Watanzania na kwamba haoni shida kubadilisha viongozi kwani lengo ni kufanya kazi nzuri kwa moyo mkuu na moyo mmoja. Tukawajibike kwa wananchi.

