Na Lucy Ngowi
MIGOGORO na Mashauri 16 kutoka kwenye Kanda mbalimbali nchini, yamepokelewa na kushughulikiwa na Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi na Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari, Ufundi Stadi na Utafiti (RAAWU), kwa mwaka 2023/2024.
Katibu wa Elimu RAAWU, Baraka Shekimweri, ambaye anamwakikisha Katibu Mkuu wa chama hicho, Joseph Sayo ameeleza hayo alipozungumza na Mwandishi wa MFANYAKAZI, Mkoani Dar es Salaam.
Shekimweri amesema kati ya migogoro na mashauri hayo waliyofikishiwa, migogoro mitatu ilipatiwa ufumbuzi kwa wanachama kulipwa stahiki zao, na mmoja kuamriwa kurudi kazini.
Amesema mgogoro baina ya Lucy Manoni dhidi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Kanisa la Uinjilisti Mbalizi, ya kumwongezea mafao ya kustaafu ulikwisha baada ya kanisa kukubali kumuongezea sh. Milioni moja.
Vile vile mgogoro baina ya Kampuni ya UPSOS dhidi ya RAAWU, uliohusu upunguzaji wa wafanyakazi, baada ya kwenda Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), usuluhishi uifanyika na kuubaliana wafanyakazi kulipwa maslahi bora.
Pia mgogoro baina ya Audax Mrema dhidi ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam(DIT), wa kuingilia mfumo wa mitihani, umekamilika na mwanachama hana hatia hivyo anaendelea na kazi yake.
Amesema migogoro na mashauri mengine yapo katika hatua mbalibali za kisheria, mingine Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, kukata rufaa Tume ya Utumishi wa Umma, kuitwa kamati ya uchunguzi na mengine bado yanafanyiwa uchunguzi.
Amesema migogoro hiyo iliyopokelewa ni kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Mashariki na Kanda ya Kati.