Na mwandishi wetu
DAR ES SALAAM: MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umeanza kutekeleza maagizo ya serikali ya kuanza kulipa mafao kwa kutumia utaratibu wakotoo kilichoboreshwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema hayo kwenye semina ya kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuishi baada ya kustaafu kwa wastaafu watarajiwa wanaochangia PSSSF.

“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ilisikia kilio cha wastaafu, na leo hii ninapenda kutangaza rasmi kwamba hadi kufikia Novemba 19, 2024 jumla ya wastaafu 10,414 ambao wamestaafu kuanzia Julai 2022 na kuanza kulipwa kwa kutumia kikokotoo kile kilicholeta taharuki wameshalipwa mapunjo na kazi bado inaendelea,” amesema.
Amesema wastaafu wapya 2,479 ambao wamestaafu kuanzia Julai mosi mwaka huu, 2024 wameshalipwa mafao yao kwa kutumia kikokotoo kipya kilichoboreshwa na kazi bado inaendelea.
Pia serikali imeridhia maboresho mengine yafanyike kuanzia Januari mwaka ujao 2025.
Maboresho hayo ni pamoja na kwa wastaafu wengi wameliokuwa wakipokea kile kima cha chini cha kiasi cha sh. laki moja, sasa kuanzia pensheni ya Januari 2025 pensheni yao ya mwezi itaongezeka kutoka Sh. laki moja hadi Sh. 150,000.

“Na Wastaafu ambao walikua wakipokea pensheni ambayo ni zaidi ya Sh. 150,000 na wao watapewa ongezeka la asilimia mbili kila mmoja.
“Katika maboresho hayo, pia mstaafu yoyote anayepokea pensheni katika Mfuko wa PSSSF akifariki, Mfuko utatoa kiasi cha Sh.500,000 kwa ajili ya maziko huku Mstaafu yoyote akifariki wategemezi wake wanaotambulika na sheria ya Mfuko watalipwa mkupuo wa miezi 36 wa pensheni ya mwezi ya mstaafu husika.
“Utaratibu huu ulishaanza tangu Julai 2022 lakini ulikuwa unatumika kwa wastaafu waliokuwa wanalipwa kwa kikokotoo kipya, lakini sasa utaratibu huu unafunguliwa kwa wastaafu wote hadi wale waliolipwa kwa kutumia vikokotoo vya zamani vya kwenye mifuko iliyounganishwa,” amesema.
Ridhiwani amewahakikishia wastaafu kuwa ustahamilivu wa Mfuko wa PSSSF umeendelea kuimarika kutoka asilimia 22 hadi kufikia asilimia 36.4 hivi sasa.
Awali akimkaribisha Waziri Ridhiwani, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru, amesema, tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa PSSSF tayari umelipa jumla ya mafao yenye kiasi cha Sh. Trilioni 10.46 kwa wanufaika 310,458.

“Kwa kiasi hiki kilicholipwa ndani ya miaka sita ya Mfuko, kinaonesha haja ya kuandaa mpango wa mafunzo maalumu kwa ajili ya Wanachama wake wanaotarajia kustaafu ndani ya kipindi cha miaka miwili.
“Mafunzo haya yatalenga maeneo ya uwekezaji katika viwanda vidogo vidogo na vya kati, uwekezaji katika masoko ya fedha, kilimo biashara na ujasiriamali kwa ujumla.