Na Lucy Ngowi
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru amesema wamewezesha usafirishaji wa tani milioni 5.5 za mazao mbalimbali yakiwemo, mbogamboga, matunda, mikunde na viungo yenye thamani ya dola bilioni 6.6 sawa ns Sh. Trilioni 15.6.
Profesa Ndunguru amesema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya ya Mimea Mei 12, mwaka huu 2025 katika Viwanja vya Makumbusho ya Azimio La Arusha mkoani Arusha.
Amesema pia mamlaka hiyo imewezesha kuimarika kwa miundombinu ikiwemo ndege nyuki 21, mashine za maabara za uchambuzi wa masailia ya viuatilifu kwenye mazao ili mazao yakidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa na ndege ya kunyunyizia viuatilifu.
Vile vile amesema mamlaka hiyo imewezesha upatikanaji wa uhakika wa takwimu za mazao ya kilimo kupitia kitengo cha intelijensia ya usalama wa afya ya mimea pamoja na hifadhi ya nasaba za mimea zaidi ya aina 10,000 za mazao ya asili.
Amesema siku hiyo ya Kimataifa ya Afya ya Mimea kimsingi ilitokana na Azimio lililoletwa na nchi ya Zambia la kuanzisha maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea.
Amesema azimio ambalo lilipata uungwaji mkono na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, huku nchi za Bolivia, Finland, Pakistan, Ufilipino na Tanzania zikitia saini Azimio hilo.
“Umoja wa mataifa ulianzisha maadhimisho haya ili kuongeza kiwango cha ufahamu na uelewa kidunia kuhusu jinsi ambavyo kukinga afya ya mimea kunavyoweza kusaidia kuondoa njaa, jinsi kunavyoweza kupunguza umasikini, jinsi kunavyoweza kulinda bayoanuai na mazingira na jinsi kunavyoweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi,” amesema.
Ndunguru amesema maadhimisho hayo ya Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea mwaka huu 2025, yana kauli mbiu isemayo, ‘Umuhimu wa Afya ya Mimea katika Afya Moja’, kauli inayoweka msisitizo wa jinsi mimea yenye afya njema ilivyo muhimu kwa maisha ya binadamu, wanyama na mazingira.