Na Lucy Ngowi
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru, amesema dunia inaweza kusonga mbele katika uzalishaji endelevu wa chakula endapo itawekeza katika sayansi, teknolojia, sera imara na ushirikishwaji wa makundi muhimu katika sekta ya kilimo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Profesa Ndunguru amesema maono hayo ameyaeleza kwa kina katika kitabu chake kipya cha ‘Mageuzi ya Kilimo Duniani, Safari ya Utoshelevu wa Chakula, Uendelevu na Teknolojia’ ambacho kimeandikwa kwa lengo la kusaidia watunga sera,
Pia viongozi wa juu wa serikali, wataalamu wa kilimo, wapangaji wa mipango na taasisi za kimataifa kama Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Muungano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA) na Kituo cha Kimataifa cha Kilimo Tropik (CIAT).

Amesema kitabu hicho kinajibu swali muhimu linalolikabili dunia kwa sasa, “Tutawezaje kuwalisha watu zaidi ya bilioni 10 bila kuathiri uwezo wa sayari yetu kuzalisha chakula kwa vizazi vijavyo?,” amehoji.
Amesema kwa kutazama historia ya kilimo tangu binadamu walipoanza kulima zaidi ya miaka 12,000 iliyopita hadi hatua za kisasa za viwanda, kitabu kinatoa mwelekeo wa nini kifanyike ili kuleta mageuzi ya kweli katika sekta hiyo.
Profesa Ndunguru anasema alitumia mwaka mmoja kukiandika kitabu hicho ambacho kimechapishwa na kampuni ya Visionaly Publishers ya Marekani, na kitapatikana kupitia majukwaa makubwa ya mauzo mtandaoni, ukiwemo Amazon.
Amesema kimegawanywa katika sura 17, kila moja ikigusa eneo maalumu la mustakabali wa kilimo.
Ameeleza kuwa kitabu hicho kinachambua hali halisi ya kilimo duniani, changamoto zake na namna ya kukabiliana nazo, huku kikipa uzito mkubwa kwa matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuongeza tija.
Amezungumzia teknolojia za umwagiliaji, utafiti wa mbegu, ufuatiliaji wa mabadiliko ya tabianchi, kuongeza thamani ya mazao, matumizi ya mifumo ya taarifa za kilimo na kilimo makini.

Sera thabiti na utawala bora navyo vimetajwa kama nguzo muhimu kuelekea mageuzi ya kilimo, huku akibainisha kuwa mabadiliko hayawezi kufanikiwa endapo sera zitabadilika mara kwa mara au zikakosa uthabiti.
Amegusia pia athari za sera za kimataifa kutoka mashirika kama Benki ya Dunia na FAO katika kukuza au kudumaza juhudi za kilimo katika nchi zinazoendelea.
Katika kitabu hicho ameweka mkazo wa uwekezaji katika kilimo, akibainisha kuwa sekta hiyo haiwezi kukua bila uwepo wa mitaji kutoka serikali, sekta binafsi na taasisi za kimataifa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuunganisha ubunifu na sera ili kuleta matokeo ya pamoja badala ya kutumia mbinu moja moja zisizoendana.
Vijana, ambao kwa sasa wanakadiriwa kufikia bilioni 1.2 duniani, wametajwa kama kundi lenye nguvu kubwa ya kuleta mageuzi ya kilimo.
Ameeleza changamoto zao, kama uhaba wa mitaji na kushirikishwa kwao katika maamuzi, na vilevile teknolojia zinazoendelea kuwavuta kuingia kwenye kilimo cha kisasa na endelevu.
Amesemq Wakulima wadogo ambao nchini Tanzania wanakadiriwa kuwa kati ya asilimia 70 hadi 80 ya wakulima wote ni nguzo muhimu ya mageuzi ya kilimo kwa kuwa ndio wamiliki wakuu wa ardhi na wahifadhi wa mazingira.
Kitabu kinajadili changamoto zao na namna ya kuzivuka ili kuongeza uzalishaji na ustahimilivu.
Ameeleza pia umuhimu wa wanawake katika kilimo, akibainisha kuwa licha ya kuwa nguvu kazi kubwa, wameendelea kukumbana na vikwazo kama umiliki mdogo wa ardhi, upatikanaji wa mitaji na kushiriki katika maamuzi.
Amesisitiza kuwa bila kuwawezesha wanawake, mageuzi ya kilimo hayawezi kufanikiwa.
Masuala ya masoko na biashara ya mazao pia yametiliwa mkazo, akieleza kwamba kila nchi inapaswa kuchunguza mienendo ya masoko ya dunia, kuondoa vikwazo vya biashara na kuboresha mfumo wa mauzo ya mazao ili kukuza uchumi wa kilimo.
Katika muktadha wa mabadiliko ya teknolojia, Profesa Ndunguru amebainisha umuhimu wa mafunzo endelevu kwa watafiti, maofisa ugani na wataalamu wa sekta, akisema sayansi na teknolojia vinabadilika kwa kasi na hivyo kunahitajika mfumo wa mafunzo endelevu.
Ameeleza matokeo yanayoweza kupatikana endapo mageuzi hayo yatafanyika ikiwemo ongezeko la tija, maendeleo ya kiuchumi, ustawi wa jamii na uhakika wa chakula.
Kitabu kimegusia pia umuhimu wa kilimo endelevu kinachozingatia mazingira, uchumi na jamii, pamoja na majukwaa bunifu ya wadau yatakayowezesha teknolojia kufika kwa walengwa.
Katika mwonekano wa kilimo cha miaka 100 ijayo, ameweka taswira ya matumizi ya akili bandia (AI), roboti, kompyuta zenye uwezo mkubwa, mifumo ya utabiri wa tabianchi, uchambuzi wa udongo, na udhibiti wa magonjwa na wadudu kupitia teknolojia za hali ya juu.
Profesa Ndunguru amesema kitabu hicho tayari kinaendelea kutafsiriwa katika lugha 10, ikiwemo Kiswahili na Kifaransa, ili kuwafikia wadau wengi zaidi duniani.
Anaongeza kuwa tarehe ya uzinduzi itatangazwa mara tu mgeni rasmi atakapothibitisha.

