Na Mwandishi Wetu
GEITA: SERIKALI inaendelea kuboresha utendaji kazi wa Polisi Kata na Shehia kwa kuwajengea vituo vya Polisi na kuwapatia vitendea kazi zikiwemo pikipiki nchi nzima ili watekeleze majukumu yao kwa urahishi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema hayo Mkoani Geita katika hafla ya kukabidhi pikipiki 50 zenye thamani ya Tsh Milioni 175 zilizotolewa na mgodi wa Geita Gold Mine (GGML).
Amesema Serikali inatambua kazi nzuri inayofanywa na Polisi Kata na Shehia kwa kuwa wamesaidia kuimarisha usalama katika jamii.

Masauni amesema serikali kupitia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya mwaka 2024/2025 imepanga na kutenga bajeti ya Bilioni 224 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili kukamilisha, kuendeleza na kuanza ujenzi wa ofisi, vituo na makazi ya askari.
Pia kuongeza vitendea kazi vya kisasa katika kutoa huduma ikiwemo magari, pikipiki, boti na helkopta.
“Hadi sasa, Serikali imenunua Magari 384 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za Polisi kuanzia Makao Makuu ya Polisi hadi Wilaya, pikipiki 107 kwa ajili ya Polisi Kata na Shehia nchi nzima ikiwa ni lengo la Serikali kuhakikisha Jeshi la Polisi linapata vitendea kazi vya kutosha katika ngazi zote,” amesema.
Kwa upande mwingine Waziri Masauni amewapongeza mgodi wa Geita Gold Mine (GGML), na wadau wote ambao wamekuwa wakishirikiana na Wizara kupitia Jeshi la Polisi kwa kutoa michango mbalimbali ya kuliwezesha Jeshi hilo kutimiza majukumu yake ya kusimamia usalama wa raia na mali zao.
Naye Makamu wa Rais wa Geita Gold Mine, Terry Strong amesema anatarajia pikikipi hizo zitumike katika utoaji huduma za Polisi kwa wananchi katika maeneo ambayo yamekuwa hayafikiki kwa urahisi.
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela ameshukuru mgodi huo kwa namna ambavyo wamekuwa wakitumia sehemu ya faida yao kuboresha taasisi za Serikali ikiwemo Jeshi la Polisi ambapo leo Kukabidhiwa pikipiki 50.
Pia Mkuu wa Sera Mipango na Bajeti wa Jeshi la Polisi, Justus Kamugisha ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, amesema pikipiki hizo zinakwenda kusaidia Polisi Kata 50 huku akibainisha kuwa Mkoa huo una idadi ya Kata 123.