Na Lucy Ngowi
DODOMA: WAZIRI Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, ameitaka jamii kuacha kusubiri matukio maalumu ya viongozi ili kuanza kupanda miti, na badala yake kufanya zoezi hilo kuwa endelevu kama sehemu ya maisha ya kila siku, hatua itakayosaidia juhudi za Serikali katika kutunza na kulinda mazingira nchini.
Pinda ameyasema hayo leo Februari 6, 2026 jijini Dodoma wakati wa zoezi la upandaji miti 1,000 lililofanyika katika eneo la Njedengwa, mkoani Dodoma.
Zoezi hilo lilihusisha Taasisi ya Habari Conservation, wakazi wa eneo hilo pamoja na wanafunzi kutoka shule mbalimbali.
Amesema jamii haipaswi kusubiri matukio maalumu, kama vile siku za kuzaliwa za viongozi, ili kuanzisha kampeni za upandaji miti, bali ihakikishe kuwa kupanda na kutunza miti kunakuwa tabia endelevu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Wananchi kuanzia ngazi ya kata hadi taifa kwa ujumla tunapaswa kuwa na utaratibu wa kupanda miti bila kusubiri msukumo kutoka kwa viongozi.
“Mfano, siku ya kuzaliwa ya Rais isiwe kigezo pekee, bali tujitoe wenyewe kila wakati,” amesema Pinda.
Ameongeza kuwa lengo ni kuona kila Mtanzania anatambua umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti ya aina mbalimbali, ikiwemo ya kivuli na ya matunda, ili kuchangia kuboresha hali ya hewa na ustawi wa maisha ya jamii.
Aidha, amemshauri Mkuu wa Mkoa wa Dodoma pamoja na Taasisi ya Habari Conservation kutumia vikundi vya vijana, hususan wale wanaofanya mazoezi ya asubuhi kama kukimbia, kuwahamasisha kushiriki katika kampeni za upandaji miti katika maeneo mbalimbali.
Pinda amesema vijana wana nguvu na ushawishi mkubwa katika jamii, hivyo wakitumika ipasavyo wanaweza kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika suala la uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kudhibiti Manunuzi ya Umma (PPRA), Dennis Simba, ameipongeza Taasisi ya Habari Conservation kwa kujikita katika masuala ya mazingira kwa lengo la kuisaidia Serikali kuboresha na kutunza mazingira.
Simba amesema PPRA imeingia makubaliano ya udhamini wa mwaka mmoja na taasisi hiyo baada ya kujiunga na mfumo wa NesT unaotumiwa na Serikali katika manunuzi.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo utawezesha kuhakikisha miti iliyopandwa katika eneo la Njedengwa na maeneo mengine inatunzwa ipasavyo.
Amesema kwa sasa PPRA imekuwa mdau mkubwa wa mazingira, na akaziomba taasisi nyingine kujiunga na mfumo wa NesT ili kwenda kidigitali, kuboresha uwazi katika manunuzi na kushiriki katika shughuli za kijamii ikiwemo uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema mkakati wa mkoa ni kuhakikisha maeneo yote yaliyoainishwa yanapandwa miti kwa lengo la kutunza mazingira na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema katika msimu uliopita mkoa ulifanikiwa kupanda miti 40,000, huku matarajio yakiwa ni kuongeza idadi hiyo katika misimu ijayo ili kufikia malengo ya mkoa katika uhifadhi wa mazingira.
Naye mwakilishi wa Taasisi ya Habari Conservation, Loyce Obongo, amesema taasisi hiyo imejipanga kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine katika kutekeleza miradi ya upandaji na utunzaji wa miti, kwa lengo la kuboresha mazingira na kuhamasisha jamii kuchukua wajibu wao.

