Na Mwandishi Wetu
DODOMA: OFISI ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imekabidhi Juzuu za Toleo la Urekebu wa Sheria la mwaka 2023 kwa Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango mkubwa wa Ofisi hiyo katika mchakato wa urekebu wa sheria.
Akikabidhi nakala hizo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka, Sylvester Mwakitalu, Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Urekebu, Tafiti na Mafunzo, Rehema Katuga, amesema ushirikiano uliotolewa na Ofisi ya Mashitaka ulikuwa wa kipekee na umechangia kwa kiasi kikubwa kukamilika kwa kazi hiyo ya kihistoria.

“Wakati tunaanza kazi hii tulikabiliwa na uhaba wa watumishi, hasa mawakili, lakini tuliomba msaada kutoka Ofisi ya Mashitaka na kwa kweli walijitokeza na kutusaidia hadi kukamilika kwa kazi hii,” amesema.
Aliongeza kuwa, licha ya nakala zilizotolewa kuwa chache kutokana na gharama, zinatarajiwa kuwa nyenzo muhimu za mwanzo kwa Ofisi hiyo. Pia aliwashauri watumie nakala laini zinazopatikana kupitia mfumo wa OAG MIS Library.
Katuga amebainisha kuwa tayari maandalizi ya Urekebu wa kila mwaka kwa 2024 na 2025 yameanza, ili kujumlisha marekebisho ya sheria yanayofanywa na Bunge kila mwaka. Alisema baada ya miongo kumi, toleo lingine litatolewa lakini kazi haitakuwa nzito kama miaka iliyopita.
Kuhusu changamoto za matumizi ya toleo jipya, Katuga amesema baadhi ya wadau wamekuwa wakihitaji mafunzo kutokana na mabadiliko ya mpangilio wa vifungu na namba, ikilinganishwa na toleo la mwaka 2002. Amesema OCPD inapanga kutoa mafunzo ya kina kwa mawakili na wadau wengine ili kuwajengea uelewa.
Aidha, pamoja na nakala tano za juzuu hizo, OCPD imeikabidhi Ofisi ya Mashitaka tuzo maalum kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kutambua mchango wao kwenye zoezi hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashitaka, Sylvester Mwakitalu, ameishukuru OCPD kwa kazi kubwa na kwa kuwapatia nakala hizo ambazo amesema ni nyenzo muhimu kwa utendaji wao wa kila siku.
“Tunazitumia sheria hizi kila siku kwenye Mahakama za Wilaya, za Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani. Kupata nakala hizi kumeepusha gharama kubwa ambazo tungezitumia kununua,” amesema.
Amesema nakala hizo zitasambazwa kwa mawakili wa serikali waliopo mahakamani huku wakisubiri kupata nyingine kwa njia rasmi, pamoja na kutumia toleo la kielektroniki lililopo kwenye mfumo.
Toleo la Urekebu wa Sheria la 2023 lilizinduliwa rasmi na Rais. Samia Suluhu Hassan mwezi Aprili mwaka huu, na litaanza kutumika rasmi Julai mosi,, 2025, likifuta rasmi toleo la mwaka 2002.