Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) ni mhimili muhimu, wa lazima katika mchakato mzima wa utungaji, urekebishaji na ufasili wa sheria nchini,
Hivyo bila ofisi hiyo hakuna sheria inayoweza kuwasilishwa bungeni kwa ajili ya kutungwa.

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amesema hayo alipotembelea banda la OCPD katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Dkt. Ndumbaro amesema OCPD ndiyo inayoratibu mchakato wa kuandaa miswada, kuifanyia marekebisho na kuifasili kwa lugha nyepesi na ya kueleweka kwa wananchi.

“Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria ni kiungo muhimu katika mchakato wa utunzi wa sheria kuu na ndogo. Bila ofisi hii hakuna sheria itakayokwenda bungeni, hakuna urekebishaji wa sheria wala ufasili wake. Ni ofisi ya msingi katika mfumo wa sheria wa nchi,” amesema.
Amesema kuwa ofisi hiyo pia ina jukumu la kufasili sheria kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili, jambo linalowezesha wananchi wengi zaidi kuelewa sheria zinazowaongoza. Kufikia Juni 30 mwaka huu 2025, tayari sheria 300 kati ya 446 zimefasiliwa na kazi hiyo inaendelea.
“Kwa sasa wanafanya kazi nzuri ya kuhakikisha sheria zote zinapatikana kwa lugha ya Kiswahili. Hii itarahisisha upatikanaji wa haki na uelewa wa sheria kwa wananchi,” amesema.

Dkt. Ndumbaro ameeleza kuwa Serikali imetenga fedha za kutosha katika mwaka huu wa fedha ili kuhakikisha kazi ya ufasili wa sheria zote inakamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu wa kalenda, ikiwa ni hatua muhimu ya kuweka sheria katika lugha ya Taifa kwa matumizi ya wote.
Kwa upande wake, Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD, Philemon Mrosso, amesema ofisi hiyo inashiriki maonesho ya SABASABA kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mchakato wa utungwaji wa sheria pamoja na kuelezea majukumu yake.
“Tunawahamasisha wananchi kushiriki katika uundwaji wa sheria kupitia wawakilishi wao bungeni na pia kutoa maoni kuhusu sheria zinazowagusa moja kwa moja. Tumepokea maoni mengi na tutaendelea kuyachakata kwa ajili ya maboresho,” amesema Mrosso.
Amesema ofisi hiyo ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha ufasili wa sheria zilizobaki pamoja na kanuni zake ili zipatikane kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu 2025 kwa matumizi rasmi.