Na Lucy Ngowi
DODOMA: MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Hassan Saidy amesema kufikia mwaka 2034, zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanaweza kuwa wanatumia nishati safi ya kupikia, kutokana na mipango madhubuti ya Serikali na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika.
Akizungumza katika maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane 2025 yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma, Saidy amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imeanza kutekeleza kwa vitendo Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi kwa kipindi cha zaidi ya miaka minne sasa.

Amesena juhudi hizo zimehusisha uwekezaji mkubwa wa rasilimali fedha, muda na teknolojia, hatua ambayo imeongeza mwamko wa wananchi kutumia teknolojia za kisasa za nishati safi.
Amewashauri Watanzania kuchagua aina ya nishati safi inayolingana na uwezo wao wa kifedha, kwani fursa za kuchagua zipo.
“Nishati safi ni pamoja na umeme, gesi ya majumbani, gesi asilia, mkaa mbadala, kuni mbadala na gesi vunde. Aina hizi zinapatikana lakini matumizi yake yanategemea hali ya uchumi wa mtu binafsi. Ndiyo maana tunasisitiza watu kuchagua kwa uangalifu kulingana na uwezo wao,” amesema.

Ametaja baadhi ya miradi mikubwa iliyotekelezwa na Wakala huo ikiwemo, Kuwezesha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutumia nishati safi ya kupikia katika kambi 22 nchini, kwa gharama ya Sh. Bilioni tano.
Uwezeshaji wa maeneo 211 ya Jeshi la Magereza kutumia nishati safi, kwa gharama ya Sh. Bilioni 35.2.
Kusaini mkataba na Kampuni ya Taifa ya Madini (STAMICO) kwa ajili ya uzalishaji wa mkaa mbadala.
“Hii inaonesha dhamira ya Serikali kuhakikisha taasisi zake nazo zinakuwa mfano katika matumizi ya nishati safi,” amesema.
Amehamasisha wananchi kutembelea banda la REA lililopo katika eneo la Wizara ya Nishati, Hema Na. 2 (Government Pavilion No. 2), upande wa Kusini Mashariki wa viwanja vya maonesho ya Nzuguni, ili kupata elimu kuhusu nishati safi na teknolojia zake.
Ameeleza pia kuhusu fursa zinazotolewa na Serikali kupitia REA, ikiwa ni pamoja na utoaji wa mikopo nafuu kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa vituo vidogo vya bidhaa za mafuta (Petroli na Dizeli) vijijini, pamoja na maendeleo makubwa ya usambazaji umeme katika vijiji na vitongoji nchini kote.