Na Mwandishi Wetu
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), unaingia makubaliano na mawakala nchini ili kufanikisha usajili wa wananchi wengi zaidi.
Mkurugenzi Mkuu NHIF, Dkt. Irene Isaka amesema hayo katika Kikao Kazi kati ya mfuko huo, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA), pamoja na Mawakala nchini.
Amesema usajili kwa njia ya mawakala unatarajiwa kuanza Februari mwaka huu 2025, ambao utawafikia wananchi katika maeneo yote nchini.
Amesema serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanakuwa ndani ya Mfumo wa Bima ya Afya hivyo Mawakala watasaidia kufikia malengo hayo.
“NHIF tumeona umuhimu wa kufanyakazi kwa kushirikisha mawakala ili wananchi waweze kufikiwa walipo na kusajiliwa kwenye bima ya afya ili waweze kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha.
“Kwa kaya zisizo na uwezo, Serikali imeweka mazingira wezeshi ili nao wapate Bima ya Afya. Nawaomba sana tuunge mkono juhudi za Serikali chini ya uongozi mahiri wa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kuwa na Bima ya Afya kwa wote,” amesema.
Kwa upande wa mawakala hao, kwa pamoja wameupongeza Mfuko kwa hatua ya kuwashirikisha katika eneo la kuwafikia wananchi lakini pia maboresho makubwa ambayo yamefanyika katika mifumo yake na vifurushi vipya ambavyo vina huduma nyingi ikilinganishwa na awali.