Na Mwandishi Wetu
MOROGORO: MWONGOZO wa Mafunzo Elekezi kwa walimu wanaoajiriwa kwenye Utumishi wa Umma, umeandaliwa ili kuondoa utofauti katika kuwaelekeza walimu wapya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Profesa Maosud Muruke amesema hayo wakati akifungua kikao kazi mkoani Morogoro.
Profesa Muruke amesema maboresho ya mwongozo huo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya utumishi wa walimu nchini.
“Mwangozo umetoa maelekezo mahsusi kwa walimu wapya kuhusu misingi ya utumishi wa umma na utumishi wa walimu, haki na wajibu wao pamoja na miiko na maadili katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na taratibu zingine,” amesema.
Naye Katibu wa TSC Paulina Nkwama amesema kuwa mwongozo utawasaidia walimu wanaoajiriwa katika utumishi wa umma Tanzania Bara kupata uelewa mzuri wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia utumishi wa umma kwa ujumla na hususani katika utumishi wa walimu.
Amesema walimu wataweza kufahamu haki, wajibu, maadili yanayoongoza utumishi wa umma na taaluma ya kada yao kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi na hivyo kuwa na Utumishi wa umma wenye tija na utoaji wa huduma bora kwa wateja.
Pia mwongozo huo unalenga kuwapatia walimu wapya taarifa za msingi kuhusu haki na wajibu wao kama watumishi wa umma, kuwawezesha kufahamu mbinu bora za kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuwasisitiza umuhimu wa kujitambua kama watumishi wanaowajibika kwa jamii.
Ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha walimu kuhusu taratibu za kupanda madaraja, taratibu na hatua mbalimbali za kinidhamu, na umuhimu wa kudumisha uadilifu katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.