Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, limemwokoa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbezi Wilayani Ubungo, Dar es Salaam kutoka mikononi mwa mtekaji.
Kamanda Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema mwanafunzi huyo ( 8), wa darasa la pili Machi 6, mwaka huu 2025 alitekwa na mtuhumiwa Stanley Ulaya (18), Mkazi wa Kata ya Nguruka, Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Amesema mtuhumiwa huyo alitenda tukio hilo wakati mwanafunzi huyo aliposhuka katika daladala kabla ya kuingia katika geti la shule ndipo alipokamatwa na mtuhumiwa huyo na kumpeleka Wilaya ya Bagamoyo Pwani.
“Mtuhumiwa alikaa naye vichakani huku akitumia namba ya simu ya mzazi iliyokuwa kwenye madaftari kupiga huku akidai pesa kwa vitisho ili amuachie na asimdhuru mtoto huyo,” amesema.
Amesema jeshi hilo lilifanya kazi ya ziada ya ufuatiliaji na Jana Machi nane, majira ya saa moja usiku baada ya mtuhumiwa kukamatwa na kufikishwa Kituo cha Polisi Osterbay alijaribu kutoroka kwa kukimbia.
Amesema alipigwa risasi mguuni na kwenye paja na kufanikiwa kumzuia baada ya kutotii tahadhari za risasi zilizopigwa hewani wakati anakimbia.
“Hali yake ni mbaya na alipelekwa hospitali kwa matibabu, aidha hali ya mtoto ni njema na uchunguzi zaidi wa madaktari unaendelea,” amesema.
Amesema jeshi hilo linalaani vikali vitendo vya wizi wa watoto na aina yoyote ya utekaji na halitakuwa na huruma kwa wahusika kuwashughulikia vikali lakini kwa mujibu wa sheria.