Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: “Kipindi cha sasa hivi watu wanapenda chakula kinachotokana na mimea kwa sababu kina kiwango kidogo sana cha lehemu ‘cholesterol’ au hamna kabisa,”.
Mwanafunzi wa Mwaka wa nne kutoka Ndaki ya Sayansi na Teknolojia na Chakula, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM) Joviet Kaijage amesema hayo katika Maonesho ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu yaliyoanza chuoni hapo.
Amesema kutokana na kupenda chakula kitokanacho na mimea, ameweza kufanya utafiti wa kutengeneza nyama ya mimea yenye mchanganyiko wa mbaazi na soya.
Joviet ambaye pia yupo Idara ya Sayansi ya Chakula na Teknolojia, amesema katika utafiti wake ameangazia eneo la kiafya zaidi jinsi watu kwenye ulaji wanapendelea nini.
Amesema chakula kisichokuwa na lehemu kinapunguza magonjwa ya moyo, masuala ya saratani baada ya kula nyama kwa muda mrefu sababu ya lehemu.
” Kwa hiyo ukiangalia kanuni niliyoitumia katika mchanganyiko huo wa nyama ya mimea, nimetumia mbaazi na soya.
” Mbaazi inapatikana pia Tanzania nimeweza kuiongezea thamani kwa kutengenezea nyama hiyo. Hii nyama inaliwa na watu wasiotumia nyama ya wanyama na wanaoitumia,” amesema.
Amesema hivi sasa watanzania ndio wameanza kuipata elimu ya kwamba kumbe kuna nyama ya mimea.
“Nyama Ya mimea ina faida, walaji watapata virutubisho kama ile wanavyopata kwenye nyama ya mnyama.
” Kwa hiyo protini ipi, vitamin ipo. Madini ya chuma yapo,” amesema.
Amesema kwenye utafiti wake huo anatumua njia za kimaabara.