Na Mwandishi Wetu
DODOMA: MGOMBEA urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim, amesema atabadilisha hadhi ya Mkoa wa Dodoma kuwa Jiji lenye Makao Makuu ya nchi.
Mwalim ametoa kauli hiyo jimboni Mvumi wakati akiendelea na mikutano ya kampeni, akisisitiza kuwa makao makuu ya nchi yanapaswa kuwa na barabara za lami na majengo ya kisasa.

“Sitaki kuona vumbi ndani ya Mkoa wa Dodoma… hapa patakuwa na hadhi ya jiji, nendeni mkatuamini na kutuchagua,” amesema.
Amebainisha kuwa barabara hizo zitafika hadi mashamba ya zabibu ili kurahisisha usafirishaji wa mazao kwenda viwandani kwa ajili ya uchakataji.
Katika hatua nyingine, Mwalim amesema sera ya CHAUMMA ni kuwarejeshea wananchi ardhi yao iliyochukuliwa na serikali kwa kuongezwa kama hifadhi au vinginevyo.
“Wananchi wote walionyangan’ywa maeneo ya pembezoni mwa hifadhi tutawarejeshea,” amesema.