Na Mwandishi Wetu
WATU wawili Ally Mwakilembe (45), Mkazi wa Kijiji cha Kapeta Kata ya Ikinga Tarafa ya Bundali Wilaya ya Ileje, Songwe na Wema Ndile (32), wamefariki dunia kutokana na wivu wa mapenzi.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Johnny Maro imesema Oktoba 15 mwaka huu saa 4:30 usiku Kijiji cha Kapeta, Mwakilembe alimshambulia kwa kumchoma visu Wema sehemu za shingoni na ubavuni upande wa kulia akiwa nyumbani kwake na kusababisha kifo chake.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya tukio hilo Mwakilembe naye alijichoma kisu tumboni na kujisababishia jeraha ambapo alikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Ileje, Oktoba 17 mwaka huu saa 9:30 alfajiri alifariki akiwa anaendelea na kupatiwa matibabu hospitalini hapo.
“Mwakilembe na Wema walikuwa ni mke na mume na walitengana miezi mitano iliyopita ambapo mke aliamua kwenda kuishi sehemu nyingine,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa ilisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linatoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi ili kuepusha kutokea kwa matukio mabaya kama hayo ya mauaji.